Arusha. Wazalishaji wa mbegu katika nchi za Afrika wametakiwa kuzalisha mbegu zinazozingatia ubora na zilizofanyiwa utafiti, ili wananchi wapate lishe bora na kutokomeza utapiamlo unaosababishwa na lishe duni.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Aprili 7, 2025 na Mratibu wa Utafiti wa Mazao kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Dk Atugonza Bilaro, akizungumza wakati wa uzinduzi wa benki mpya ya mbegu iliyofadhiliwa na Taasisi ya Kimataifa ya The Alliance of Bioversity International and CIAT kwa kushirikiana na Tari.
Amesema benki hiyo ni muhimu kwa usalama wa chakula na kwamba wazalishaji wa mbegu wakizingatia matumizi ya mbegu zenye ubora na zilizofanyiwa tafiti, watasaidia kuongeza lishe bora na kutokomeza utapiamlo.
“Uwepo wa benki hii ni muhimu, lazima wakulima watumie mbegu bora zisizo na magonjwa na zitawapatia kipato kwani kilimo ni biashara. Wakitumia mbegu bora zilizofanyiwa tafiti watakuwa na uhakika wa kipato, lakini pia itaongeza usalama wa chakula,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya The Alliance of Bioversity International and CIAT, Dk Juan Lucas amesema benki za mbegu ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambapo dunia inapokabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Ndiyo maana tunafanya tafiti na kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika tafiti ili kuweza kuzalisha mbegu zinazoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza usalama wa chakula na ustahimilivu wa mifumo ya chakula,” amesema.
Mwakilishi wa taasisi hiyo hapa nchini ambaye pia ni mtafiti, Sylvia Kalemera amesema hapa nchini wamekuwa na miradi mbalimbali ikihusisha utafiti wa maharage.
“Tunajua wakulima wengi wa maharage wanatumia mbegu wanazotoa sokoni na za muda mrefu, na kama zilitolewa na utafiti, zilitolewa kwa ajili ya mahitaji ya wakati ule. Tunajua hali ya hewa na mahitaji ya soko yamebadilika.
“Tunafanya kazi na Tari kuvumbua mbegu mpya ambazo zinaendana na hali ya hewa na soko la wakati huu. Lengo ni kumuwezesha mkulima apate mbegu zitakazoleta uzalishaji mkubwa, lakini akishapata uzalishaji mkubwa atapata chakula na kipato, ataboresha afya yake na kipato chake,” amesema.