Cadena, Simba ni suala la muda tu

KLABU ya Simba iko mbioni kuachana na kocha wa makipa wa timu hiyo, Dani Cadena baada ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu huu.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimeiambia Mwanaspoti kwamba, Cadena hana mpango wa kuongeza mkataba mwingine licha ya viongozi wa Simba kupambana kumuongezea mwaka mmoja zaidi.

“Alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Simba kukiwa na kipengele cha kuongeza mwingine ila yeye mwenyewe ameonyesha kwamba hayupo tayari kuendelea nasi kwa msimu ujao japo viongozi wanapambana kwa ajili ya kumbakisha,” kimesema chanzo chetu.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema suala linalohusu maboresho ya mikataba ya benchi la ufundi au wachezaji liko chini ya uongozi na hawana presha yoyote kwa sababu watakaowataka wataendelea kubaki nao msimu ujao.

Cadena alipotafutwa na Mwanaspoti, amesema kwa sasa nguvu na akili zake ameziwekeza kwa ajili ya kumalizia michezo ya Ligi Kuu Bara iliyobaki na baada ya hapo ndipo ataweka wazi juu ya hatima yake ndani ya kikosi hicho.

Licha ya kauli hiyo, lakini mtu wake wa karibu ameiambia Mwanaspoti kwamba kocha huyo hayupo tayari kubaki Tanzania huku sababu kubwa ikielezwa ni kutokana na umbali alionao na familia yake yenye makazi nchini Hispania.

Cadena, raia wa Hispania alijiunga na Simba Julai 6, mwaka jana baada ya kuachana na kikosi cha Azam FC kufuatia mkataba wake kwisha akichukua nafasi ya raia wa Morocco, Chlouha Zakaria aliyeondolewa.

Kocha huyo aliyezaliwa Januari 3, 1978 katika kisiwa cha Baleares huko Mallorca, Hispania ni msomi wa mpira wa miguu mwenye leseni ya Uefa Pro ambayo ndio kubwa zaidi barani Ulaya  na amewahi kufanya kazi katika klabu za Sevilla, Real Betis na Recreativo Huelva.

Mara ya kwanza Cadena alitua nchini na kujiunga na Azam Julai Mosi, 2022. Pia aliwahi kufanya kazi pia klabu za Guangzhou Mingtu na Shanghai Jiading za China akiwa na uzoefu mkubwa na elimu ya juu ya Shirikisho la Soka la barani Ulaya (UEFA).

Related Posts