Watu 249 wachunguzwa na kutibiwa moyo Zanzibar

…………….

Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

07/04/2025 Watu 249 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo iliyofanyika kwa siku nne katika uwanja wa Amaani uliopo Zanzibar.

Hayo yamesemwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aika Nnkya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi hiyo ya upimaji na matibabu ya moyo.

 

Dkt. Aika alisema kati ya watu 249 waliowafanyia uchunguzi watu 199 walikutwa na matatizo ya moyo hii ni sawa na asilimia 80 ya watu wote waliowaona ambapo watu 77 sawa na asilimia 31 hawakuwa wanajijua kuwa na matatizo ya moyo.

 

“Wagonjwa 22 ambao tumewakuta na matatizo ya moyo ya kuziba kwa mishipa ya damu, mfumo wa umeme wa moyo na valvu tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu ili tuwafanyie uchunguzi zaidi”.

“Ninatoa wito kwa wananchi zinapotokea nafasi za upimaji kama hizo wajitokeze  kwa wingi kupima afya zao kwa mfano katika kambi hii watu waliokutwa na matatizo  wametibiwa na kupewa dawa za kutumia mwezi mmoja bila malipo yoyote yale” alisema Dkt. Aika.

Kwa upande wake mratibu  wa kambi hiyo ya matibabu daktari bingwa wa moyo kutoka  hospitali ya Rufaa Lumumba Khamis Mustafa alishukuru kuwepo kwa kambi hiyo na kusema kuwa imesogeza kwa karibu huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi.

“Ninazishukuru sana Idara za Habari maelezo kwa kuja na wazo hili katika mkutano wao kuwepo na huduma ya upimaji na matibabu kwa wananchi kwani wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) , Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wametoa huduma za matibabu ya magonjwa  mbalimbali”.

“Ninaomba kambi hii ya matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali ambayo inahusisha hospitali hizi kubwa tatu iwe endelevu kwani inawasaidia wananchi kupata huduma za matibabu ya kibingwa kwa wakati na bila gharama yoyote ile tofauti na ambavyo wangezifuata Dar es Salaam”, alisema Dkt. Ndiz.

Nao wananchi waliopata matibabu katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma walizozipata na kusema kuwa zimwewasaidia kufahamu hali za afya ya miili yao na wengine kupata matibabu kutokana na matatizo waliyokuwa nayo.

“Ninaishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutuletea wataalamu hawa mimi nilikuwa nikilala moyo wangu unakwenda kasi sana baada ya kufanyiwa uchunguzi nimeambiwa moyo wangu unashida kidogo nimepewa dawa za kwenda kutumia”, alishukuru Halima Shaaban mkazi wa Mwera.

“Baada ya kusikia kuna huduma za matibabu nilikuja hapa kutibiwa kwani mimi ninatatizo la mgongo na presha , nimefanyiwa vipimo na kupewa dawa za kwenda kutumia ninashukuru sana na ninawaomba wananchi wenzangu wachangamkie fursa hii ya matibabu pindi inapotokea”, alisema Juma Abdala mkazi wa Makunduchi.

Huduma hiyo ya matibabu ilitolewa kwa wananchi za Zanzibar na washiriki wa kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali kilichoandaliwa na Idara za Habari – Maelezo za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mwisho

 

Related Posts