Matarajio ya wadau ziara ya Rais Samia Angola

Dar es Salaam. Kuimarisha ushirikiano, kukuza biashara, mustakabali wa kinachoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa katika ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Angola.

Kwa mujibu wa wadau tofauti, ziara hiyo mbali na kukuza uwekezaji na biashara baina ya mataifa hayo mawili, pia, inatarajiwa kutengeneza msingi wa mpango wa maridhiano DRC.

Matarajio hayo ya wadau yanakuja ikiwa leo Aprili 7, 2025, Rais Samia ameanza ziara yake ya siku tatu nchini Angola, alikokwenda kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, João Lourenço.

Katika ziara hiyo, Rais Samia atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Lourenço, kuhutubia Bunge la Angola, kuweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu wa mwasisi wa Taifa hilo, hayati António Agostinho Neto na kutembelea Kiwanda cha Mafuta cha Luanda.

Pia, kutakuwa na uwekaji saini wa Hati za Makubaliano (MOU) katika masuala yanayolenga kufungua fursa za biashara na uwekezaji na jitihada za kuimarisha ulinzi na usalama.

Aidha, Rais Samia amealikwa na Spika wa Bunge la Angola, Carolina Cerqueira kuhutubia Bunge la nchi hiyo.

Ikumbukwe kwamba ziara hiyo inakuja miaka 19 tangu Rais wa Tanzania kufanya ziara za kiserikali nchini humo, huku ziara ya kwanza ilifanywa na Baba wa Taifa.

Baadaye alifuatiwa na Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, mwaka 2006, alihutubia Bunge la nchi hiyo kama Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

Akizungumzia hilo, mwanazuoni wa uchumi, Profesa Benedict Mongula amesema kwa jumla ziara ya mkuu wa nchi katika Taifa fulani ina faida za kiuchumi, biashara na hata uhusiano.

Kama nchi anayokwenda Rais inafanya biashara, alisema Taifa litanufaika kwa kujenga uhusiano ya kibiashara utakaohusisha kuuziana bidhaa mbalimbali.

“Kama anakokwenda ni matajiri, Taifa linatengeneza uhusiano na kuimarisha urafiki utakaowezesha baadaye kupata misaada kwa urahisi,” amesema.

Lakini ziara ya Rais Samia nchini Angola, amesema inaweza kuwa ya kimkakati hasa ukizingatia katika siku za karibuni kumeibuka mambo mbalimbali.

Miongoni mwa mambo hayo ni vita vinavyoendelea mashariki mwa DRC, ambayo Angola imeonyesha maslahi yake.

“Pengine nchi hiyo imetaka kukutana na Rais Samia kwa kuwa ni kiongozi wa idara ya amani katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), hivyo wanataka kuzungumza kuhusu maridhiano nchini DRC,” amesema.

Jambo lingine, amesema katika siku za karibuni, viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani kutoka Tanzania walizuiwa kuingia nchini humo, akisema huenda likawa moja ya mambo watakayokwenda kujadili.

“Angola iliwazuia baadhi ya viongozi wa upinzani kutoka Tanzania na maeneo mengine, pengine wanataka kwenda kuzungumza kidiplomasia na kushauriana kati ya Serikali na Serikali,” amesema Profesa Mongula.

Akizungumza baada ya kuwasili nchini Angola kwa ajili ya ziara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Kombo amesema ziara hiyo ni ushirikiano wa kweli ambao lazima ujikite kwenye maeneo yenye fursa halisi za kiuchumi, kijamii na kidiplomasia.

“Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa maeneo tutakayojadili katika ziara hii yanaakisi malengo ya kimaendeleo ya nchi zetu. Tuangalie maeneo yenye tija ya moja kwa moja kwa wananchi wetu,” amesema.

Amewataka wajumbe kutoka taasisi na wizara mbalimbali za Tanzania kutumia fursa hiyo kuchambua kwa kina maeneo yatakayochangia kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuinua maisha ya wananchi kupitia ushirikiano wa kimkakati.

“Ziara hii ya kihistoria ya Rais Samia inatarajiwa kuleta matokeo makubwa, siyo tu kwa upande wa uhusiano wa kidiplomasia, bali pia katika kutafsiri kwa vitendo fursa zilizopo kwa manufaa ya wananchi wetu,” amesema Waziri Kombo.

Kwa upande wa mwanazuoni wa historia katika siasa, Philemon Mtoi amesema imepita miaka 19 tangu Rais wa mwisho azuru nchini Angola, ilhali ni Taifa ambalo Tanzania ina urafiki nayo toka kitambo.

Kwa sababu ya uhalisia huo, amesema ililazimika kwa mkuu wa nchi kufanya ziara katika taifa hilo hasa ukizingatia amepokea mwaliko kutoka kwa Rais wa Angola.

“Angola ni miongoni mwa nchi tulizozisaidia kupata uhuru, ili kudumisha mahusiano nayo ni vema wakuu wa nchi wawe wanafanya ziara,” amesema.

Amesema Angola ni miongoni mwa mataifa yenye ushawishi katika siasa za Afrika, hivyo ziara ya Rais Samia inaweza kutengeneza nafasi ya kujenga ushawishi kwa mgombea wa Tanzania katika nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Profesa Mohamed Janabi.

Related Posts