Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema ipo haja ya kuanzisha mpango wa ujuzi wa vijana wa Jumuiya ya Madola utakaosaidia kuwapatia ujuzi zaidi ya vijana milioni moja katika sekta ya uchumi wa buluu na kijani ifikapo mwaka 2030.
Dk Mwinyi amesema hayo leo Aprili 7, 2025 alipozungumza katika Mkutano wa Biashara na Uwekezaji wa Jumuiya ya Madola unaofanyika London, Uingereza.
Amehimiza kuanzishwa kwa ufadhili wa kujitolea na utaalamu katika sekta hiyo ili kuharakisha maendeleo endelevu ya bahari katika nchi za Jumuiya ya Madola.

“Mpango huu utasaidia kukuza ujuzi kwa vijana katika sekta ya uchumi wa buluu na vijana wengi zaidi watanufaika nao,” amesema Dk Mwinyi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Dk Mwinyi amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2050 Zanzibar itakuwa ya uchumi wa kati baada ya kuzinduliwa Dira ya Maendeleo kupitia mkakati wa sera ya uchumi wa buluu ya mwaka 2022.
Ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kuitembelea Zanzibar kujionea fursa za uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu, utalii wa mazingira, nishati mbadala ya bahari, ufugaji wa samaki endelevu na maendeleo ya bandari.
Katika mkutano huo, mazungumzo kwa watunga sera yatajikita zaidi kupunguza vizuizi kwa biashara ya Jumuiya ya Madola, kufungua uwekezaji katika masoko ya ukuaji, akili mnemba na mabadiliko ya nishati ya ulimwengu.

Mkutano huo wa kila mwaka, unaofanyika leo Aprili 7 hadi 8, ukikusanya jamii ya wafanyabiashara wa Jumuiya ya Madola na wakuu wa Serikali, mawaziri wakuu na wawakilishi wa Serikali wanachama wa jumuiya hiyo.
Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi amesema Serikali inatambua mchango wa Jumuiya za Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) kwa kuwekeza nyumbani Tanzania na kuisemea nchi katika kuhamasisha utalii kwa wageni.
Amesema hayo alipozungumza na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Uingereza Aprili 6, 2025.
Amewahakikishia kuwa Serikali itakuwa pamoja nao kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili kwa maendeleo ya nchi.
Dk Mwinyi ametoa wito kwa diaspora kuendelea kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali na kuwekeza katika hatifungani ya Zanzibar SUKUK.
Vilevile, amewaeleza kuwa Serikali itaendelea kuwatumia wataalamu wa fani mbalimbali wanaoishi nje ya Tanzania kuja kufanya kazi nchini.
Rais Mwinyi amewasisitiza kuendeleza utamaduni, mila na desturi za Kitanzania na kutoiga mila za kigeni.
Mbali ya hayo, Rais Mwinyi amezindua tovuti maalumu ya Tanzania link portal ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza itakayotoa fursa za biashara, uwekezaji, ufadhili wa elimu ya juu na ajira.