KenGold na Dakika 180 za kubaki Ligi Kuu

KABLA ya kumalizika kwa mwezi huu, tunaweza kuishuhudia KenGold ikilazimika kuanza harakati za kujiandaa kushiriki Championship msimu ujao endapo itashindwa kuzitumia vizuri dakika 180 zijazo sawa na mechi mbili.

Kwa sasa KenGold ina hali mbaya zaidi ikiwa kwenye harakati za kupambana kubaki Ligi Kuu Bara, huku hatma yao kwa asilimia kubwa ikiwa mikononi mwa Tanzania Prisons na Coastal Union.

Timu hiyo yenye maskani yake jijini Mbeya, imepanda daraja kushiriki Ligi Kuu Bara msimu huu, hivyo inapambana mechi tano zilizobaki kutetea nafasi yao inayoweza kuipoteza kabla ya kuingia mwezi ujao.

Kupoteza mchezo uliopita kwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, kumezidi kuichimbia shimo timu hiyo ambayo ina kibarua cha Jumatano hii kupambana na ndugu zao wa Mbeya, Tanzania Prisons ambao nao hawapo sehemu nzuri wakipishana pointi tano zikiwa nafasi ya 16 na 15 kwenye mstari wa kushuka daraja moja kwa moja.

Baada ya hapo, Mei 21 mwaka huu KenGold itakwenda Tanga kukabiliana na Coastal Union iliyotoka kuachana na Kocha Juma Mwambusi huku ikiwa nayo haina uhakika wa kubaki kwenye ligi ikiwa na pointi 25 nafasi ya 13 kabla ya mechi yao na Yanga na ipo katika mstari wa kucheza mechi za mtoano kuwania kubaki kwenye ligi.

Kwa pointi 16 ilizonazo KenGold ikiwa nafasi ya mwisho kwenye msimamo, zinawalazimu kushinda mechi mbili zijazo dhidi ya Tanzania Prisons na Coastal Union ili kufikisha 22 ambazo angalau bado zitawaweka kwenye uhai, lakini ikiwa tofauti, ijiandae na Championship.

Ipo hivi; KenGold katika mechi tano zilizobaki, kama ikishinda zote itafikisha pointi 31 ambazo hivi sasa inazo Dodoma Jiji na JKT Tanzania zilizopo nafasi ya saba na sita, lakini ikipoteza mbili zijazo, itakuwa na uwezo wa kumaliza ligi na pointi 25 zilizokusanywa na timu iliyopo kwenye mstari wa kucheza play-off ya kuepuka kushuka daraja.

Ratiba ya mechi za KenGold zinaifanya timu hiyo kuwa na mlima mrefu kwani mechi tatu zijazo itacheza dhidi ya timu zilipo nafasi nne juu yake ambazo pia zinapambana zisishuke daraja huku mbili ikicheza nyumbani na moja ugenini.

Timu hizo ni Tanzania Prisons yenye pointi 21 katika nafasi ya 15, Coastal Union ipo nafasi ya 13 na pointi 25 na Pamba Jiji iliyo nafasi ya 12 ikikusanya pointi 26.

Baadaye ya itaikaribisha Simba, timu inayopambana na Yanga katika kuwania ubigwa wa ligi, kisha itamalizana na Namungo ugenini.

Kagera Sugar iliyopo nafasi ya 14, inahitaji pointi tisa pekee ili kutopitwa na KenGold hata ikishinda mechi zote tano wakati Coastal Union inayokamata nafasi ya 13 na pointi 25, inahitaji pointi sita pekee kuinyima fursa KenGold kuwa juu yao, huku timu zote zikibakiwa na mechi tano zenye pointi 15.

Related Posts