Watoto 18 kutoka mazingira magumu wajifunza Kichina

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiingiza lugha ya Kichina kwenye mitaala ya masomo ili ifundishwe shuleni, tayari watoto wa Kitanzania wamefadhiliwa kusoma bure lugha hiyo.

Watoto hao 18 wanaotoka katika mazingira magumu, wanafadhiliwa kujifunza lugha hiyo na Chama cha Mabuddha cha China kilichopo hapa nchini, ambapo wakimaliza itawawezesha kupata kazi ili wajikimu kimaisha.

Hayo yamebainishwa kwenye sherehe za Kimataifa za kuzaliwa kwa Buddha nchini Tanzania zilizofanyika jana Jumapili Mei 19, 2024 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watoto hao pamoja na wadau mbalimbali kutoka nchini China.

Akieleza zaidi, Mwalimu Mkuu wa Shule inayowafundisha watoto hao ya LongQuan Bodhi, Jane Shao amesema lengo ni kuwawezesha watoto wa Kitanzania kujifunza lugha za kimataifa zitakazowawezesha kupata ajira katika nchi tofauti tofauti.

“Shule hii imeanza mwaka huu ‘2024’ inawanoa wanafunzi wa Kitanzania 18, pia inamiliki kituo cha watoto wanaotoka katika mazingira magumu kinachoitwa Longquan Bodhi Children Care Centre.

“Wanafunzi wanafundishwa tamaduni za kichina, matarajio yetu katika miaka mitatu ijayo tutafungua shule ya sekondari kisha chuo cha ufundi,” amebainisha.

Amesema malengo ya wawekezaji hao kutoka China ni kujikita katika maadili ambayo watoto wa Kitanzania wataweza kujitegemea kuanzia kifikra.

Akitaja mafanikio, amesema watoto hao 18 wameshajua lugha ya Kichina na sasa wanachanja mbuga katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

“Lengo la kuanzisha shule hii ni kuwawezesha wajue lugha ya Kichina, ili wawe watoto wa kimataifa na waweze kuzunguka mataifa tofauti tofauti wapate ajira,” amesema.

Amesema kuna mtoto mmoja anayetoka mazingira magumu atasafiri kwenda China, kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Kitaifa yaitwayo Chinese Bridge Competition.

Akizungumza mtoto huyo aitwaje Tausi Julius, amesema anayofuraha kujua lugha ya Kichina na anaamini itamsaidia katika maisha yake kwa kupata ajira.

“Nimejifunza Kichina na sasa niko tayari kufanya kazi ya kuwafundisha wasiokifahamu lakini pia nimepata maarifa,” amebainisha Tausi.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa Shule hiyo Master Xian Hong, amesema kwa sasa kuna miradi mingi ya Kichina inaendelea nchini hivyo watoto hao ni rahisi kupata kazi katika utekelezaji wake.

Amesema faida yake pia watoto hao wanajifunza tamaduni za Kichina, jambo linaloongeza ushirikiano kati ya nchi hizo ambazo zina uhusiano wa kirafiki kwa zaidi ya miaka 60.

“Watoto wetu hawa wanapata ujuzi, lakini pia watakuwa mabalozi wa kueneza tamaduni za kichina katika nchi nyingine ambapo ni faida kwao kwasababu itakuwa ni kazi,” amesema Master Hong.

Related Posts