KLABU ya Yanga leo imetoa ratiba ya sherehe zake za ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Mei 25, mwaka huu zikiongozwa na paredi kutoka Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam hadi makau ya klabu hiyo, Jangwani.
Awali Yanga iliwasilisha maombi kwa Bodi ya Ligi (TPLB) kuomba michezo miwili dhidi ya Tabora United na Tanzania Prisons kukabidhiwa kombe la ligi, lakini sasa itapewa Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ally Kamwe amesema kombe hilo watakabidhiwa Mei 25 baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United.
Kamwe amesema baada ya kukabidhiwa ubingwa, Mei 26 wataanza sherehe hizo kuanzia Uwanja wa Mkapa hadi Jangwani.
“Kabla ya kupewa Kombe letu siku hiyo ya mechi asubuhi kutakuwa na burudani ya kutosha kutoka kwa wasanii wakubwa. Tukitoka hapo tutaingia uwanjani, baadaye kutakuwa na pati, siku inayofuatia asubuhi tutakunywa supu kama kawaida Jangwani kisha tunaanza kumtembeza mwali wetu kwa Mkapa hadi Jangwani,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa kabla ya sherehe hizo Mei 22 watakuwa na mchezo dhidi ya Dodoma Jiji ambao umepewa jina la kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi.
“Kesho tunasafiri majira ya saa nne asubuhi kuelekea pale mkoani Dodoma kucheza dhidi ya Dodoma Jiji. Mechi hii ya Dodoma tumeifanya mechi ya kushukuru benchi la ufundi, hivyo itakuwa ni Gamondi Day,” amesema.
“Kwenye Gamondi Day itakapofika dakika ya 30, wana Yanga wote tunapaswa kusimama kumpigia makofi Gamondi na benchi lake la ufundi kwa dakika moja. Tunampa heshima kwa kutupatia ubingwa wa kihistoria mara ya 30”
Kuhusu viingilio vya mchezo dhidi ya Tabora United amesema VIP A tayari tiketi zimeshaisha, VIP B Sh10,000, VIP C 5,000 na mzunguko 1,000.