Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amehimiza kukamilishwa kwa haraka kwa mradi wa ujenzi wa hotel ya nyota tano mkoani humo inayojengwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Mtanda amesema hayo leo Mei 12, 2024 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo, huku akisisitiza kwamba ni azma ya Serikali kuona miradi ya kimkakati ukiwemo wa ujenzi wa hoteli hiyo inakamilika kwa wakati na kutoa huduma kwa wananchi.
“Nawapongeza NSSF kwa kazi nzuri na ubunifu mkubwa wa miradi ya kimkakati wanayoitekeleza sehemu mbalimbali nchini. Nawaomba waendelee kuongeza kasi ya utekelezaji ili ile azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuona miradi hii inakamilika kama ilivyokusudiwa,” amesema.
Amesema mradi wa NSSF wa hoteli ya nyota tano jijini Mwanza utakapokamilika, utaongeza thamani katika jiji hilo, amewahakikishia NSSF kwamba serikali ya mkoa itaendelea kutoa ushirikiano kwao ili kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuanza kutumika kama ilivyokusudiwa.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji, Mapesi Maagi amesema uwekezaji wa mradi huo ni moja kati ya majukumu manne ya mfuko huo ambayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.
Maagi amesema uwekezaji wa hoteli hiyo utakapokamilika utachochea maendeleo ya Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kwa kuinua shughuli za kiuchumi hususan utalii hasa ukizingatia kuwa Mwanza imepakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ipo karibu na mkoa huo.
Naye, Meneja wa NSSF Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Kahensa amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufanya ziara hiyo ya kikazi katika mradi huo wa hoteli ya nyota tano.
Akitoa taarifa ya mradi, Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi Helmes Pantaleo amesema utekelezaji wa mradi na changamoto zote zilizokuwa ni kikwazo zimetatuliwa. Amesema utekelezaji unaendelea na kwamba mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2024 na kuanza kazi Machi 2025.