Ufunguzi wa kongamano la siku(2) la kitaifa la mtandao wa wanawake katiba uongozi na uchaguzi

Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP katika mchakato kuhimiza  usawa wa kijinsia Tanzania imekutana na wanawake pamoja na wanamtandao katika kongamano la kitaifa la mtandao wa wanawake katiba uongozi na uchaguzi Kujadili masuala mbalimbali wakati ambapo hivi sasa nchi yetu inaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo hali ya ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ikiwa bado iko chini sana .

Kulingana na TGNP takwimu za hali ya ushiriki wa wanawake kwenye ngazi zote za uongozi kwa wanawake kisiasa bado upo chini ukilinganisha na wanaume, kwa mfano; Wabunge wa kuchaguliwa Majimboni Wanawake ni 26 kati ya 264, Wenyeviti wa kijiji ni 2.1%, 246/11915, serikali ya mtaa, 12.6%, vitongoji 6.7% ya wenyeviti wote.

Hivyo basi jitihada za makusudi, bado zinahitajika kutoka katika ngazi zote, wadau,azaki,mitandao,serikali, jamii hadi Taifa ili haki za wanawake na vijana wa kike kushiriki katika uongozi na michango yao katika masuala ya mikakati ya kisiasa vitambulike na kuthaminiwa zaidi.

Kongamano hili la siku mbili la TGNP, linatoa uwanda mpana wa majadiliano, tafakari na kujikumbusha kuhusu umuhimu wa nguvu ya pamoja, kubainisha mapungufu na mafanikio yaliyojitokeza yanayotokana na jitihada za nguvu za pamoja katika kuhakikisha kuwa sauti za wanawake wote hususan walio pembezoni zinajitokeza na kusikika kwa wingi katika mwendelezo wa kupigania ajenda ya ukombozi wa mwanamke kimapinduzi hususan tunapoelekea katika chaguzi muhimu za Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.

Prof .Penina Mlama , Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake Katiba Uongozi na Uchaguzi amesema matumaini makubwa ya kongamano hilo ni kutoka na mikakati wezeshi iliyojikita katika kuimarisha Mtandao wao wa (TAPO) katika (umiliki wa pamoja wa ajenda;utetezi na ushawishi wa ajenda) katika muktadha mzima wa demokrasia shirikishi kwenye ngazi mbalimbali kwa kipindi chote cha uchaguzi na kuendelea.

”Napomaliza salama hizi za ufunguzi, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa niaba ya Mtandao kwetu sote kwa kufika kwa wingi katika kongamano hili. Vilevile kipekee niwashukuru Mfuko wa Ruzuku kwa Wanawake Tanzania (WFT-T) kwa kuendelea kufadhiri na kuratibu shughuli za Mtandao kwa kushirikiana na Kamati ya Kitaalam ya Mtandao.’

”Pia natoa rai kwa Serikali na wadau wote kwa ujumla kuweka mazingira wezeshi na salama kwa wanawake na watu wenye ulemavu, na kuhakikisha kuwa wadau wote wa uchaguzi wanazingatia misingi ya ushindani wa haki huru na usawa wa jinsia kama ilivyoainishwa kwenye katiba, sheria, sera na mipango ya nchi”.

”Vilevile natoa wito kwa Wanamtandao wote na Wanawake kwa ujumla kuendelea kushiriki na kujitokeza kwa wingi katika kuendeleza harakati za ukombozi wa mwanamke kufikia rasilimali za kitaifa na kijamii, kushiriki kikamilifu katika maamuzi muhimu ya kitaifa mathalani mchakato wa kutoa maoni kuhusu (Dira ya Maendeleo ya Uchumi wa Taifa 2050) unaoendelea katika kupanga mipango ya pamoja na kuingizwa misingi ya haki za wanawake kwenye muktadha za kiuchumi,kijamii na kisiasa itakayopelekea Maendeleo na Ustawi wa  wanawake hapa nchini”.

Related Posts