Walichosema viongozi wa kanisa, mazishi ya askofu aliyejinyonga

Dodoma. Viongozi wa dini waliofika kwenye ibada ya mazishi ya msiba wa aliyekuwa askofu mkuu wa makanisa ya Methodist Tanzania, Joseph Bundala wamewataka waumini wa kanisa hilo kuwa na uvumilivu kwenye kipindi hiki cha msiba na kumwachia Mungu kazi ya kuhukumu.

Viongozi hao wametoa kauli hiyo leo Jumatatu Mei 20, 2024 kwenye ibada ya mazishi ya askofu huyo ambaye alifariki Dunia Mei 16 mwaka huu kwa kujinyonga ofisini kwake.

Akizungumza kwenye ibada hiyo Msaidizi wa Askofu kutoka dayosisi ya kati, Askofu Daudi Samweli amesema kilichotokea ni maamuzi binafsi ya Askofu Bundala na siyo msimamo wa kanisa.

Amelitaka kanisa lisitetereke katika kipindi hiki cha msiba wala wasirudi nyuma kwani imani ni lazima iendelee kulindwa kwani kilichotokea kimeshatokea na hawawezi kubadilisha matokeo.

“Tumesikitika sana kutokana na tukio hili lakini tumwachie Mungu ajuaye ndiye atoe hukumu kwa kuwa hakuna mtu asiyekuwa na dhambi na ndiyo maana Yesu alikufa,” amesema Askofu Samweli.

Kwa upande wake Askofu wa kanisa la Christian Methodist, Fabian Kikopo amesema hakuna sababu ya watu kuhukumu tukio la kifo cha Askofu Bundala kwani naye alikuwa ni mwanadamu kama walivyo wanadamu wengine na kulitaka kanisa kutokata tamaa Bali wasonge mbele katika imani na msiba huo uwaimarishe zaidi badala ya kuwagawanya.

Naye mwenyekiti Mstaafu wa umoja wa makanisa ya Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Peter Konki amesema kila mtu ana njia yake ya kwenda mbinguni hivyo linapotokea jambo la mauti ni kweli linaumiza lakini halina budi kutokea na badala ya kuanza kuhukumu watumie nafasi hiyo kumtafuta Mungu zaidi.

“Hata katika hili bado tunaendelea kuiamini kuwa Mungu atabaki kuwa Mungu, hivyo tusirudi nyuma tuendelee kumwamini Mungu.

Msiba huo umehudhuriwa na viongozi wa madhehebu mbalimbali, viongozi wa serikali na wamiliki wa shule binafsi Mkoa wa Dodoma.

Related Posts