Na Mwandishi Wetu, Tabora
Chacha ametoa onyo hilo wakati akizungumza na wakulima wa vyama vya msingi vya ushirika vya wakulima wa tumbaku, baada ya kutembelea maghala ya Kampuni ya Alliance One Tobacco Limited, (AOTL) kujionea uwekezaji mkubwa na mwenendo wa soko la tumbaku.
Amesema kuna baadhi ya wakulima wanafanya vitendo vya udanganyifu kwa kuchanganya tumbaku nzuri na mbaya, na wengine wanatorosha tumbaku badala ya kuuzia kwenye vyama vyao walivyokopea na kujisajali ambako wanadaiwa madeni yao ya pembejeo.
‘Serikali yenu ya mkoa imeanza kuchukua hatua, nadhani mmesikia….na tutaendelea kuchukua hatua kwa yeyote atakayejaribu kuwahujumu Wakulima wenzake” amesema Chacha.
Amesema uchumi wa mkoa wa Tabora unategemea kilimo cha tumbaku, hivyo serikali ya mkoa itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha wakulima, ambao wengi ni vijana, ili waendelee kuzalisha bila vikwazo vyovyote hasa pembejeo na masoko.
Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya AOTL, David Mayunga, amesema uwekezaji wa ujenzi wa maghala ya kuuzia tumbaku mkoani Tabora uliogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 26.8 ni mkakati wa kukuza uzalishaji wa zao hilo ambalo ni nguzo muhimu ya uchumi wa taifa.
Amesema lengo la kujenga maghala hayo ya kuuzia tumbaku ni kuwa na kituo kimoja cha kuuzia zao hilo tofauti na zamaini ambapo walilazimika kuwa na vituo vingi na kusababisha zoezi la ununuzi kuchukua muda mrefu uliokuwa unashusha ubora wa majani yake.
Bw Mayunga amesema uzalishaji wa tambaku msimu huu umekumbana na changamoto ya mvua nyingi iliyoathiri kiwango cha uzalishaji zikiwemo za kupotea kwa mbolea mara baada ya kuiweka kwenye mimea,kubomoka kwa mabani ya kukaushia majani ya tumbaku hali iliyosababisha baadhi ya mimea kupoteza ubora na kupungua mavuno.
Naye Meneja Mahusiano wa Kampuni ya AOTL, Wakili John Magoti amewaomba wakulima kuzingatia taratibu na sheria za uzalishaji wa tumbaku kama wanavyofafanuliwa na maafisa ughani ili kuepuka hasara kwao na kwa kampuni na kushuka kwa uchumi wa taifa.
Amesema wasipozingatia taratibu na sheria za uzalishaji wa Tumbaku watajisababishia hasara kwa tumbaku yao kukataliwa, halmashauri kukosa mapato na uchumi wa taifa kushuka na kwamba Bodi ya Tumbaku inaendelea kutoa elimu na miongozo ili kuhakikisha zao hilo linaendelea kuzalishwa kwa viwango vinavyohitajika.
Mkulima Tausi Juma wa Ibushi wilayani Nzega, amesema ujio wa masoko hayo makubwa utapunguza sana muda wa kuuza mazao yao kwa sasa tofauti n hapo awali ambapo walikuwa wanafanya mauzo kwa zaidi ya miezi miwili.
Msemaji wa Kampuni ya Tumbaku ya Alliance One, John Magoti(Katikati) akifafanua jambo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora(kushoto) wakati kiongozi huyo alipotembelea uwekezaji na maendeleo ya masoko ya ununuzi wa tumbaku mwaka huu.Kulia ni Mkurugenzi wa Uzalishaji Kampuni hiyo David Mayunga.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora(katikati) akiangalia kishada cha majani ya tumbaku wakati alipotembelea uwekezaji wa maghala na kujionea soko la tumbaku la kampuni ya Alliance One mkoani humo.Wa pili Kushoto ni Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni hiyo David Mayunga