Wafanyabiashara kurejeshewa asilimia tatu ya VAT wakiwa na nyaraka kamili

Unguja. Ili kupata unafuu wa wa kodi kwa wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa zao kutoka Zanzibar kwenda Tanzania bara au kinyume chake, wanatakiwa kuwa na nyaraka muhimu za bidhaa hizo.

Ili mfanyabiashara aweze kunufaika na nafuu ya kutolipa kodi mara mbili, ni lazima afuate taratibu za kuondosha mizigo Zanzibar na kupeleka Tanzania Bara kwa kuwa na nyaraka zote muhimu za kusafirisha mizigo hiyo zikiwemo nyaraka za kodi.

Pia, akinunua bidhaa Tanzania Bara kuipeleka Zanzibar iwapo akiwa na nyaraka zote, atarejeshewa asilimia tatu ya ongezeko la Ongezeko la Thamani (VAT).

Watarejeshewa asilimia hiyo kwa sababu Tanzania Bara kiwango cha VAT ni asilimia 18 na Zanzibar asilimia 15.

Hayo yamelezwa leo Jumatatu Mei 20, 2024 na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Juma Makungu Juma katika Mkutano wa 15 Baraza la Wawakilishi wakati wa kipindi cha maswali na majibu.

Makungu alikuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Mwanakwerekwe Ameir Abdalla Ameir, ambaye alitaka kujua kwa kiasi gani wafanyabiashara wa Zanzibar wanapata unafuu wa kodi kwa bidhaa wanazosafirisha kwenda Tanzania Bara.

Makungu amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua hatua za kutunga sera na sheria mbalimbali ambazo zinaendelea kuufanya mfumo wa kodi wa Zanzibar kuwa rafiki, rahisi wenye usawa na wenye kutabirika.

“Ili kuepuka kulipa mara mbili lazima mtu kubeba nyaraka kamili za bidhaa alizonunua lakini wengine wamekuwa wakipata usumbufu kwa sababu ya kutokuwa na nyaraka hizo,” amesema

Amesema Serikali inafanya hayo ili kuimarisha mazingira mazuri ya uwekezaji yatakayowavutia wawekezaji wa ndani na nje na kufanya biashara ndani ya Zanzibar.

Katika mnasaba huo, wafanyabiashara wa Zanzibar ambao wanachukua bidhaa Zanzibar na kuzipeleka Tanzania Bara kwa lengo la kutafuta soko, wanapata unafuu wa kodi kwa mujibu wa sheria za kodi ziliopo.

“Wafanyabiashara hao wanapata unafuu wa kutolipa tena kodi waliyokuwa tayari wameshalipia Zanzibar na hutatakiwa kulipa tofauti ya kodi ya asilimia tatu katika kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kodi ya Ongezeko kwa vile Tanzania Bara kiwango cha VAT ni asilimia 18,” amesema

Ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara, kufuata taratibu za kusafirisha mizigo na kuwa na nyaraka zote muhimu zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria, ili kuondokana na usumbufu wa kulipa kodi mara mbili.

Naye naibu Spika, Mgeni Hassan Juma amesema jambo hilo lina maslahi makubwa kwa wanachi wa Zanzibar na kwamba bado kuna kadhia ya watu kutozwa ushuru hata kwenye bidhaa ambazo watu wanaingiza kama kugawa sadaka akitolea mfano kuwa na yeye limewahi kumkuta

“Mheshimiwa Waziri, hili jambo lipo na umekuwa mtindo hata kama mtu analeta nguo kwa ajili ya kutoa sadaka lakini anakutana na kadhia, hili linaumiza wengi sana hata mimi limeshanikuta,” amesema

Hata hivyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesisitiza iwapo mtu akifuata utaratibu na akawa na nyaraka zote zinazotakiwa, akinunua bidhaa Tanzania bara akifika Zanzibar atarejeshewa asilimia tatu ya ongezeko hilo.

“Ukiwa na nyaraka zote, ukinunua bidhaa Tanzania bara kwa VAT ya asilimia 18 ukija Zanzibar ile asilimia tatu ukiwa na nyaraka zote utarejeshewa,” amesema.

Related Posts