Walioachwa Simba watwaa ubingwa | Mwanaspoti

TIMU ya APR imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda 2023/24 bila ya kupoteza mchezo huku kikosini kwake ikiwa na mastaa wawili walioachwa na Simba ya Tanzania ambayo jana ilifungwa mabao 2-1 na Yanga katika Kariakoo Dabi.

APR imetwaa taji hilo kwa mara ya tano mfululizo baada ya kuifunga Kiyovu Sports bao 1-0, katika mechi ya duru ya 27 ya Ligi Kuu Rwanda na kufikisha pointi 63 ambazo hakuna timu itakayozifikia kati ya 15 nyingine zinazoshiriki ligi hiyo ambapo mabingwa hao wametwaa taji hilo wakiwa na mechi tatu mkononi.

APR imetwaa ubingwa huo huku katika kikosi chake kukiwa na viungo wawili, Mganda Taddeo Lwanga na Msudani Sharaf Eldin Shiboub waliowahi kuichezea Simba kabla ya kuachwa ambapo Shiboub aliondoka Msimbazi mwaka 2020 huku Lwanga akitemwa mwaka 2022.

Ukiachana na Lwanga na Shiboub, katika kikosi cha APR msimu huu kulikuwepo na kocha wa viungo Adel Zrane aliyefariki April 2, mwaka huu. Kabla ya kutua APR, Zrane alikuwa kocha wa viungo ndani ya Simba.

Wakati wawili hao wakisherehekea ubigwa ndani ya APR, timu yao ya zamani, Simba ilikuwa uwanjani kwenye mechi ya dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga na kufungwa mabao 2-1 yaliyowekwa nyavuni na Stephane Aziz Ki kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 20 na Joseph Guede aliyeukwepa mtego wa kuotea katika dakika ya 38 huku lile la kufutia machozi kwa Simba likiwekwa nyavuni na Freddy Koublan katika dakika ya 74.

Ubingwa huo umekuwa ni wa 22 kwa APR iliyoanzishwa mwaka 1993 ikiwa ndiyo timu iliyotwaa mara nyingi zaidi ubingwa wa Ligi Kuu Rwanda ikifuatiwa na Rayon Sports iliyotwaa taji hilo mara tisa.

Related Posts