WAKALA wa Vipimo (WMA), imetoa elimu ya vipimo na kukabidhi mizani kwa wafanyabiashara wa soko la Ilala katika kuadhimisha Siku ya Vipimo Duniani.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika soko hilo leo Mei 20, 2024 Jijini Dar es Salaam, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani amewataka wafanyabiashara kuacha kucheza na vipimo kwani hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika.
Charangwa amesema kwa muda mrefu serikali imekuwa ikihimiza matumizi ya vipimo sahihi kwa wafanyabiashara kwa kutumia mizani yenye nembo ya WMA na ambayo nisahihi.
“Wafanyabiashara kwenye masoko wamezoea kutumia vipimo vya kienyeji kwa hiyo tumeanza kutoa elimu na kuwapa motisha ya mizani mitano iliyohakikiwa na WMA kwa vikundi vitano vya wafanyabiashara,” amesema
“Tunatoa wito kwa wafanyabiashara wote kuacha kutumia lumbesa na waache kuchezea vipimo kwa hiyo wananchi ombeni kupimiwa bidhaa kupimiwa kwa vipimo rasmi kwasababu hivi vya kienyeji wakati mwingine mnapunjwa,”amesema.
Aidha ameipongeza WMA kwa kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wafanyabiashara kwani inawajengea uelewa kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo ili keupuka faini.
Kwa upande wake Meneja wa WMA Mkoa wa Ilala, Muhono Nashon, amesema vipimo vingi vinatumika kwenye maeneo ya masoko na ndiyo sababu WMA imeamua kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa soko la Ilala ambapo baadhi ya vikundi vimepewa mizani ya bure kama motisha ya kutumia mizani iliyohakikiwa.
“Wale wanaochezea vipimo tunawasihi waache kwasababu sheria ya sasa ni kali na adhabu imeongezwa, tunawasihi wahakikishe mizani yao imehakikiwa kwa kuweka stika kutoka WMA, kosa moja la kuchezea mzani linaanzia faini ya laki moja hadi milioni 20 kwa hiyo mfanyabiashara akitozwa faini kama hii ni dhahiri atayumba kibiashara,” ameeleza Nashon.
Amesema uelewa kuhusu vipimo sahihi umeongezeka kwa kiwango kikubwa na wafanyabiashara wengi wameanza kutumia mizani zilizohakikiwa na wakala.
“Tunapotoa elimu hii tunataka watu wote waache kutumia vipimo vya kienyeji watumie vipimo sahihi na vilivyohakikiwa na tunapofanya msako na kukuta watu wanatumia vipimo batili tumekuwa tukitoa adhabu kali kwa hiyo wafanyabiashara wasisubiri tufanye msako wanapaswa kutii sheria,” amesema.
Mwenyekiti wa soko la Ilala, Ali Mbiku aliipongeza WMA kwa uamuzi wake wa kuwapa elimu wafanyabiashara wa soko lake ili waweze kutumia vipimo vilivyohakikiwa.
”Mimi binafsi nitaendelea kutoa hamasa kwa wafanyabiashara wa soko hili ili ufike wakati kila mmoja kwenye soko hili awe na mzani uliohakikiwa na wakala ili mnunuzi apate kiwango cha bidhaa kinacholingana na thamani ya fedha alizotoa,” amesema
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani akikabidhi mizani kwa baadhi ya viongozi wa vikundi vya wafanyabiashara wa soko la Ilala wakati wa kuadhimisha Siku ya Vipimo Duniani ambayo hufanyika Mei 20 kila mwaka.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Ilala wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani ambapo Wakala wa Vipimo (WMA) walitoa elimu ya Vipimo na kukabidhi mizani kwa wafanyabishara hao leo Mei 20, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa soko la Ilala, Ali Mbiku akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Ilala wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani ambapo Wakala wa Vipimo (WMA) walitoa elimu ya Vipimo na kukabidhi mizani kwa wafanyabishara hao leo Mei 20, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Watumishi wa Wakala wa Vipimo (WMA) wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wakiadhimisha Siku ya Vipimo Duniani ambapo wametoa elimu vipimo na kukabidhi mizani kwa wafanyabiashara wa Soko la Ilala leo Mei 20, 2024 Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)