Wafanyakazi Takwimu watakuwa kujiendeleza kielimu

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

NAIBU Waziri wa Fedha,Hamad Hassan Chande amewataka wafanyakazi wa Ofisi za Taifa za Takwimu (NBS) kufanya kazi kwa maarifa, weledi na bidii kubwa huku akiwataka kujiendeleza kielimu.

Kauli hiyo ameitoa leo Mei 20,2024 wakati akizungumza kwenye mkutano wa wafanyakazi wa Ofisi za Takwimu Tanzania Bara (NBS) na Zanzibar ( OCGS)

Mkutano huo umehudhuriwa na wakurugenzi, mameneja,wakuu wa vitengo na watumishi kutoka Ofisi za Taifa za Takwimu Tanzania Bara na Zanzibar.

Naibu Waziri Chande amesema wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii kwani hakuna haki bila wajibu.

“Niwaombe vijana wapewe fursa ya kwenda kujiendeleza kwa masomo kwani ufanisi unaongezeka.

“Yule ambaye anasema anatosha msikae mkaridhika jiendelezeni kimasomo,wapatieni motisha wale wanaofanya vizuri,”amesema Naibu Waziri huyo.

Pia ametoa wito kwa taasisi nyingine zilizopo katika wizara ya fedha kupitisha vikao kama hivyo ambavyo vinahusisha Tanzania Bara na Visiwani.

“Niwaombe sana watumishi wenzangu tuendelee kufanya kazi kwa uadilifu kwa kufuata mambo matatu la kwanza lolote unalolifanya mtangulize Mungu,la pili unapoaminiwa jiaminishe la tatu subiri kichache upate kingi,”amesema Naibu Waziri Chande.

Ameyataja mafanikio katika takwimu ni pamoja na kufanya mazoezi matatu sensa ya watu,sensa ya majengo na anuani za makazi ambazo zilifanyika kiditali na zilifanyika kwa mafanikio makubwa.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali,Dk Albina Chuwa amesema lengo la kikao hicho kujadili mafanikio na changamoto katika Ofisi za takwimu Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo bila ya takwimu kuwekwa mbele.

“Tupo hapa kwa ajili ya kuunganisha pamoja, sisi tunafanya kazi kama ndugu huwezi kutofautisha Mkurugenzi wa Tanzania Bara na Visiwani.Tunapenda tasnia ya Takwimu iendelee kupata heshima,”amesema Dk Chuwa.

Naye,Mwenyekiti wa Tugwe Tawi,Shagilu Shagilu amewataka wafanyakazi kutunza utu na uadilifu.

“Hiki ni kikao cha kipekee tangu uhuru upatikane ambapo nimekaa kwa miaka 15 hivyo ni kikao cha kipekee.Tunamshukuru Mungu kwa Rais wetu kuna namna ametuwezesha wafanyakazi ila wafanyakazi lazima tutunze utu na uadilifu nafahanu kuna namna ambavyo maokoto yameongezeka lakini yasitutoe kwenye utu,”amesema

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Salum Kassim Ally amesema mkutano huo ni adimu na adhimu kwao na watashiriki kwa ukamilifu.

“Mkutano huu uwe wa kuamsha ari hakuna aliyepata hasara ikiwa atafanya kazi kikamilifu Mkutano huu uwe wa amsha ari ili kuimarisha utoaji na uzalishaji wa takwimu.

Amesema takwimu ni tasnia mtambuka ila bado wana nafasi ya kuzalisha takwimu zenye kiwango cha Kitaifa na kimataifa.

Naye,Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara, Anne Makinda amesema lazima wafanyakazi wa takwimu wajitahidi kusoma ili wawe na ubora zaidi huku akiwataka kuwa na maadili na uaminifu.

“Kingine msikiache kabisa,uadilifu,uaminifu na ni vizuri mkawa navyo na mkavisimamia.Nyie muwe na chachu ya Nchi yetu kuwa mpya Tanzania ni yetu sote,”amesema Makinda ambaye ni Spika Mstaafu.

Mwenyekiti wa bodi ya Takwimu Zanzibar,Amina Salum Ally amesema :”Sensa imeonesha taasisi zetu zipo tayari na zinapiga hatua.Niwaombeni tusichoke”.

Related Posts