Uwanja wa Sokoine umeendelea kuwa wa bahati kwa Mashujaa baada ya leo kuikanda mabao 2-1 Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Bara na kuongeza matumaini ya kubaki kwenye ligi.
Mashujaa iliingia uwanjani ikikumbuka kuchapwa mabao 2-0 na wapinzani hao walipokutana katika mzunguko wa kwanza kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma na leo wamelipa kisasi.
Sokoine imeendelea kuwa neema kwa Mashujaa kwani wakati wanapanda Ligi Kuu Bara waling’ara kupitia uwanja huo walipoichapa Mbeya City bao 1-0 na kuishusha kupitia mchujo (play off).
Katika mchezo wa leo, Mei 20, Mashujaa walionyesha kiu ya kutaka pointi tatu ili kujiweka pazuri katika msimamo wa ligi na kufanikiwa kupata mabao mawili ya haraka katika dakika ya 14 na 19.
Mabao katika mechi hiyo yalifungwa na David Ulomi aliyeitanguliza Mashujaa kabla ya Shaban Mgandila kuweka la pili kwa penalti na kudumu hadi mapumziko.
Hata hivyo, dakika ya 39 mechi hiyo ilisimama kwa muda kutokana na kadi nyekundu ya mwamuzi Nassor Mwinchui aliyomuonyesha nahodha na beki wa Prisons, Jumanne Elfadhir, na kusababisha vurugu hadi mabenchi ya ufundi na wachezaji kuingilia kati.
Elfadhir alionekana kutokubali kadi ya kwanza ya njano baada ya refa kutafsiri kuwa alimchezea rafu mchezaji wa Mashujaa, Idrisa Stambuli na kujaribu kuhoji, lakini alijikuta akionyeshwa nyekundu hali iliyomfanya kupaniki na kuzuiwa na wachezaji wenzake uwanjani asichafue hali ya hewa zaidi.
Pia kabla ya tukio hilo, straika wa Prisons, Samson Mbangula aliangushwa nje kidogo ya eneo la hatari la lango la Mashujaa na mwamuzi kupeta na kuamsha zomeazomea kutoka kwa mashabiki wa Prisons kuwa wageni walikuwa wanapendelewa.
Licha ya kuanza kipindi cha pili wakiwa pungufu, Prisons walilazimisha mashambulizi na dakika ya 64 walipata bao baada ya beki wa Mashujaa kujifunga wakati akijaribu kuokoa mpira ilhali kipa wao, Patrick Munthali akiwa ametoka langoni.
Matokeo hayo yanaifanya Prisons kufikisha michezo tisa mfululizo bila ushindi ikiwa ni sare sita na kupoteza mitatu dhidi ya Mtibwa Sugar 2-1, Ihefu 1-0 na leo kichapo hicho na kuwa nafasi ya sita kwa alama 33.
Mashujaa ambao ni msimu wao wa kwanza katika Ligi Kuu wanafikisha pointi 29 wakibaki nafasi ya 13 na sasa wanasubiri mechi mbili dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji kujua hatima yao kwenye ligi hiyo.
Mechi ya kwanza Mtibwa Sugar ilitoka suluhu na Namungo, ikiendelea kubaki mkiani mwa ligi.