Msigwa, Sugu wanavyopishana wakisaka kura

Mbeya. Wakati Mchungaji Peter Msigwa akianza na Mbeya kusaka kura kutetea nafasi ya uenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, mpinzani wake, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ tayari amemaliza mikoa ya Rukwa na Songwe kusaka kura za wajumbe.

Uchaguzi wa chama hicho katika kanda hiyo unatarajiwa kufanyika Mei 29, 2024 katika mji wa Makambako mkoani Njombe ambapo tayari kampeni zinaendelea kwa wagombea wa nafasi mbalimbali.

Msigwa ambaye anatetea nafasi hiyo kwa muhula wa tatu sasa, amesema haamini kama wajumbe wataamua kumuondoa kwenye nafasi hiyo kutokana na mambo mengi aliyofanya katika kipindi alichokuwa kiongozi wa kanda hiyo.

Mbunge huyo wa zamani wa Iringa Mjini, tayari ameanza kampeni zake akianzia mkoani Mbeya, jana Mei 19, 2024 ambapo aliibukia katika viwanja vya Polisi Chimala wakati wa ufunguzi wa michuano ya Mwang’ombe Cup.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Msigwa amesema haamini kama wajumbe watamtosa kwani ni mengi ameyafanya kwa muda alioongoza kanda hiyo, huku akieleza kuwa akipita tena ataanza na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi ujao.

Amesema mambo anayojivunia ni kuipa nguvu na kuitangaza Kanda ya Nyasa ndani na nje, mikutano ya kisiasa, usajili wa wanachama kidigitali zaidi ya asilimia 21, uwazi, uweledi na mafunzo kwa wanachama.

“Tuna kanda 10 nchini, lakini Nyasa ndiyo kinara wa usajili kidigitali, tumekuwa mfano kutokana na uimara wa uongozi wangu, lakini hata kisiasa kanda yetu imekuwa ndiyo wa kuanza.

“Kipaumbele changu nikirudishwa tena ni kupambana na CCM kwenye uchaguzi, uwezo ninao kwani wanachama 49,000 wenye kugombea nafasi zote wapo na wengine ziada,” amesema Msigwa.

Pia, Msigwa amewaomba wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kushiriki uchaguzi ili kupata viongozi bora akieleza kuwa Chadema inaamini itafanya vizuri.

“Sisi Chadema tunaamini kwenye fursa, ninampongeza Liberatus Mwang’ombe kuandaa michezo kama hii, na leo nimeanzia Mbeya na tayari wapigakura saba nimewapata,” amesema Msigwa.

Kwa upande wake, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema tangu kupita kwenye kwenye mchakato huo, hajatulia, amekuwa akisafiri mikoa tofauti akianza na Rukwa, Songwe na sasa yupo mkoani Mbeya Wilaya za Kyela, Lupa, Busokelo na Rungwe.

Amesema anaamini wajumbe wanahitaji mabadiliko na hawaendeshwi kwa hisia za mtu mmoja, akieleza kuwa viongozi wa chama hicho wanao uwezo na uelewa katika kupata maendeleo.

“Kama nilivyoieleza Mwananchi baada ya kupita kwenye usaili, bado sijapumzika nipo nasaka kura na tayari nimemaliza Rukwa na Songwe na sasa nimefika Mbeya, kesho Iringa na Njombe, wajumbe wanataka mabadiliko,” amesema Sugu.

Related Posts