Nachingwea. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema walijua mapema kuwa wapinzani wao wasingeshiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 kutokana na mwenendo wao.
Makalla ambaye hakukitaja moja kwa moja chama hicho, ameyasema hayo leo Jumamosi Aprili 12, 2025 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi katika Uwanja wa Maulid ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
“Mko tayari kwa uchaguzi…Niwaombe muda utakapofika mkiunge mkono Chama cha Mapinduzi na leo kumetolewa taarifa, ya vyama vya siasa kusaini makubaliano ya kanuni za uchaguzi, vyama vyote mnavyovijua vimesaini makubaliano hayo maana yake ndivyo vitakavyoshiriki uchaguzi.
“Kwa bahati mbaya, lakini siyo kwa bahati mbaya, ni watu ambao waliamua mwaka huu wapumzike, hao waliokuja hapa walikuwa wamechoka sana, mwaka huu wameamua kupumzika na mimi niliwaambia hawa hawajajiandaa na uchaguzi, hawa wana migogoro na leo imethibitika, hawajaenda kusaini, maana yake hawatashiriki uchaguzi,” amesema Makalla.
Hata hivyo, Mwananchi inafahamu kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ndicho hakijashiriki hafla ya kusaini sheria za uchaguzi iliyofanyika leo katika Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma.
Makalla amewataka wanachama, wapenzi na wakeleketwa wa chama hicho kukipa kura CCM sababu ni haki yao ya msigi.
“Chama chako hakitakuwepo, wewe kapigie kura Chama Cha Mapinduzi, kwa hiyo leo ni rasmi kwamba jamaa wamekataa kusaini lakini tuliwatabiria kwamba hawajajiandaa na wanaonekana kuchoka na mtu aliyechoka hutakiwi kumlazimisha aendelee na safari. Mtu anakwambia goti linauma, mtu anakwambia pumzi inakata, hivi utaendelea kumwambia twende?” amehoji Makalla na kuongeza:
“Kwa hiyo, wenzetu wale wamethibitisha leo kwamba hawatakuwa sehemu ya vyama vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu na hata ikitokea uchaguzi mdogo hawatashiriki kwa miaka mitano,” amesema.

Ameongeza kuwa nguvu zote zilizotumiwa na chama hicho ilikuwa ni sawa na kazi bure.
“Zile mbilinge mbilinge na vichekesho walivyofanya hapa zote ni kazi bure, kwa hiyo hatuwezi kusema kwamba ndiyo timu ambayo imekimbia mechi aah, hawa walishachoka, hawawezi muziki wa Chama Cha Mapinduzi.
“Wao leo wamepoteana na wamethibitika kwa hiyo tutakuwa na vyama vingine lakini hao wengine waliokuja juzi hapa hawapo tena. Na mimi nitoe rai kwa wanachama wa chama hicho kwa sababu hawatashiriki uchaguzi basi wana uhuru wa kupiga kura,” amesema.
Amesisitiza kwamba kwa sababu walijiandikisha amewaomba kura zao wakipe Chama cha Mapinduzi muda utakapofika wa kampeni watakapopita kuomba kura zao.