Diwani Rombo ashambuliwa na wafugaji, avunjwa mkono na kujeruhiwa kichwani

Rombo. Kundi la wafugaji jamii ya Kimasai linalodaiwa kutoka nchi jirani ya Kenya, limevamia na kujeruhi watu kadhaa akiwemo Diwani wa Kata ya Marangu-Kitowo, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, Simon Rogath ambaye amevunjwa mkono na kujeruhiwa sehemu ya kichwani.

Tukio hilo lilitokea Aprili 10, 2025 wakati diwani huyo alipoitwa na wananchi wa kata hiyo, Kitongoji cha Masekini, wakiomba msaada kwake baada ya wafugaji hao kuswaga mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima ambayo yana mazao ya mahindi, karanga na mbaazi.

Alipotafutwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Raymond Mwangwala kuzungumzia tukio hilo aliomba apewe muda wa kufuatilia kujua jambo hilo limefikia wapi kwa kuwa lipo polisi.

“Nipe muda nifuatilie maana lipo polisi nitapata jibu sahihi kutoka kwao nitakupa majibu baada ya kujua wamefikia hatua gani,” amesema DC Mwangwala.

Akizungumza na Mwananchi leo, Aprili 12, 2025, diwani Rogath amesema baada ya kuitwa na wananchi wa Kitongoji cha Masekini wakitaka msaada kwake, alifika eneo la tukio na kukuta wananchi wakipambana kuondoa mifugo hiyo na tayari walikuwa wamewadhibiti kwa kuwaweka sehemu moja.

Amesema baada ya kufika eneo hilo na kukuta tayari mifugo ipo upande wa juu, yeye pamoja na watu wengine walioongozana pamoja na walikwenda upande wa mbele ili kuzuia mifugo hiyo isitolewe eneo hilo mpaka hapo sheria itakapochukua mkondo wake kutokana na uharibifu uliofanywa na mifugo hiyo.

“Ilikuwa Aprili 10 saa 1 kasoro usiku, nilipokea simu kutoka kwa wananchi wa ukanda wa chini wakiniomba niende mara moja,  wakinieleza wale wa Maasai (wafugaji) wameleta tena ng’ombe lakini tumefanikiwa kuzizuia na kwa sheria zetu za kijiji mifugo inavyokuja namna hiyo, huwa tunaichukua na kuifikisha kwenye ofisi ya kijiji ili sheria ichukue mkondo wake,” amesema Rogath.

Ameongeza kuwa: “Niliondoka kuwafuata nikiwa nimeongozana na vijana, tukaelekea eneo la Kitongoji cha Masekini (eneo ambalo lilivamiwa na mifugo) wakati nakaribia eneo la tukio, nikapigiwa simu kwamba wanataka kurudisha ng’ombe kwao.

“Nilipofika nikasema acha niendelee kufuatilia maana bado mifugo yao ilikuwa kwenye eneo letu pale Masekini, tulikaa mbele ya wale mifugo tukitaka kujua ni kwanini mifugo inarudishwa na ilikuwa kwenye uharibifu, tukasema lazima sheria ichukue mkondo wake.”

Amesema wakati wakiwa eneo la tukio kujadili ni hatua gani za kuchukua akasema gafla alivamiwa na wale wafugaji wakaanza kumshambulia kichwani kwa rungu na kisha kumvunja mkono.

“Wakati tunazungumza pale wale vijana wa kimasai walikuwa na wazee wao ambao walikuwa wamekaa eneo la juu, walikuwa na pikipiki zao wametulia huku vijana wao wanaendelea kulisha mifugo kwenye mashamba ya wananachi,” amesema diwani huyo.

Ameongeza: “Wale wazee walianza kuongea na wale vijana ghafla wakaanza kuondosha mifugo yao kuelekea ukanda wa chini sisi ambao tulikuwa mbele tukaanza kushambuliwa na fimbo, ghafla nikapigwa kichwani, wakarudia tena mara ya pili kunipiga kichwani, wakati wakiendelea kunipiga kichwani nikawa nimejikinga na mkono, ndipo waliponivunja mkono.”

Amesema wananchi wa ukanda wa chini wa kata hiyo kwa miaka mingi wamekuwa wakisumbuliwa na wafugaji hayo licha ya kwamba wamekuwa na vikao vya mara kwa mara vya ujirani mwema.

“Wenzetu hawa amekuwa na desturi kwamba kila usiku wanapandisha mifugo na kuswaga  kwenye mashamba ya wananchi na kipindi hiki ni kipindi cha palizi mahindi ni makubwa, mbaazi, karanga na maharage lakini wao jioni ni muda wa kulishia mifugo yao.

“Kwa kweli ni kipindi kirefu sana wananchi wa ukanda wa chini wanaolima mashamba Masekini pamoja na hata maeneo ya jirani ng’ombe wansumbua sana iwe ni kipindi cha kiangazi, ndugu zetu wamekuwa wakipandisha mifugo na kuharibu mashamba ya wananchi,  wananchi wamekuwa wakiteseka sana kuhusu mifugo ya hawa wenzetu,” amesema.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekitii wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Gilbert Tarimo amelaani tukio la kushambuliwa kwa kiongozi huyo na kusema halileti picha nzuri kwenye jamii.

“Tunalaani tukio hili la kushambuliwa kwa kiongozi mwenzetu, haileti picha nzuri kwenye jamii lakini hawa wenzetu tumekuwa tukikutana nao kwenye vikao vya ujirani mwema kwamba wasiwe wanaleta mifugo huku wakati wa jioni watu wameshaondoka mashambani, lakini wameendelea na mbaya zaidi imefika mahali anashambuliwa kiongozi,” amesema.

Related Posts