CCM Zanzibar yatoa onyo kwa watia nia kabla ya muda

Unguja. Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimesema hakitamvumilia mwanachama yeyote ambaye ataanza kujipitisha majimboni na kuanza kupiga kampeni kabla ya wakati.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,  Dk Mohammed Said Dimwa ametoa kauli hiyo Aprili 12, 2025 wakati akizungumza na kamati za siasa za wadi, Wilaya ya Kusini ikiwa ni ziara ya kukagua uhai wa chama na kuelezea mabadiliko ya katiba ya chama namna ya kupata wagombea na kura za maoni.

Dk Dimwa amesema chama kimetoa nafasi kuanzia Mei 1 Mosi mpaka 15 mwaka huu kwa mwanachama yeyote mwenye sifa za kugombea nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kuchukua fomu za kuwania nafasi hizo lakini bado hakijaruhusu kuanza kufanya kampeni.

Amesema yeyote atakayeingia kwenye jimbo la mwingine kwa lengo la kumfanyia fujo chama kitamchukulia hatua bila huruma.

“Naomba niseme wazi kwamba ole wake mtu yeyote atakayeingia kwenye jimbo la mwenzake kwa lengo la kumfanyia fujo naapa kwamba sitamuonea huruma mtu huyo,” amesema.

Amesema kuchukua fomu ni jambo moja, lakini kuingia katika majimbo ni jambo jingine, hivyo mtu anachukua fomu lakini anatakiwa kutulia mpaka muda utakapofika na hatakiwi kuingia katika jimbo la mwenzake wakati bado anaendelea kufanya kazi.

Amebainisha kuwa likivunjwa Bunge na Baraza la Wawakilishi ndipo itatangazwa rasmi tarehe ya kuanza kwa kampeni na hapo sasa watu wataruhusiwa kuingia majimboni.

Kwa mujibu wa Dk Dimwa, CCM kinatoa nafasi kwa kila mwanachama mwenye sifa ya kugombea nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kwenda kuchukua fomu, “Bahati nzuri sana sifa za mwanachama kuwania nafasi hizo siyo kubwa ni kujua kusoma na kuandika Kiswahili,”amesema.

“Sasa kwa yeyote anayeweza kujipima, akaona anafaa kugombea nafasi hizo kwa mwanachama yeyote, nafasi ipo wazi kuanzia Mei 1 mpaka Mei 15,” amesema.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja, Asha Mzee Omar amesema wamejipanga vizuri katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo, ameahidi kwamba wataendelea kudumisha amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Aidha taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, Aprili 10, 2025 ilieleza kuwa, “Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wanachama watachukua na kurejesha fomu kwa Katibu wa CCM wa Wilaya husika,” amesema.

Kwa upande wa viti maalumu  vya Wanawake (Bunge/Baraza la Wawakilishi) kupitia UWT na makundi maalumu (NGOs, Wafanyakazi, Wasomi na Watu wenye Ulemavu) fomu zitapatikana kwa Katibu wa UWT wa mkoa husika.

Viti maalumu vya wanawake kupitia

Jumuiya ya UVCCM fomu zitachukuliwa na kurejeshwa kwa Katibu wa UVCCM mkoa husika wakati viti maalumu vya wanawake kupitia Jumuiya ya Wazazi fomu sitatewa ofisi ya katibu wazazi mkoa.

“Wagombea udiwani wa kata (Bara) au wadi (Zanzibar) fomu zitapatikana kwa katibu wa CCM wa Kata au Wadi inayohusika na wanachama wagombea wanawake udiwani viti maalumu watachukua na kurejesha fomu kwa katibu wa UWT wa wilaya husika,” amesema.

Related Posts