Vigogo African Sports wala kiapo Championship

KATIKA kuhakikisha African Sports inakwepa janga la kushuka daraja, viongozi wa kikosi hicho wamefanya kikao cha kujadili mambo mbalimbali yanayoihusu, huku kubwa ni jinsi gani ya kukabiliana na ukata wanaokumbana nao kwa sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa African Sports, Ramadhani Sadiki alisema kutokana na hali wanayopitia waliamua kuitisha kikao na wadau, wanachama na mashabiki mbalimbali wa soka, ili kuangalia namna ya kuondokana na ukata uliopo.

“Tunashukuru muitikio ulikuwa ni mkubwa na kila mmoja wetu alijitolea kiasi cha fedha alichojaaliwa ili kuhakikisha timu inamaliza vizuri msimu huu, kama unavyojua tumekuwa na changamoto hiyo ila tunapambana kuimaliza,” alisema Ramadhani.

Mwenyekiti huyo alisema moja ya faida kubwa watakayoipata kwa sasa ni kucheza michezo yao ya nyumbani kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, hivyo itawapunguzia safari za kutoka mara kwa mara, ambazo ndizo zilizokuwa zinawarudisha nyuma zaidi.

Timu hiyo ambayo ni mabingwa wa Kombe la Muungano mwaka 1988, imepanda Ligi ya Championship msimu huu baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023 iliposhika nafasi ya 14 na pointi 23, huku msimu uliopita ikiwa ndio mabingwa wa First League.

Hadi sasa kikosi hicho kimecheza michezo 26 ya Ligi ya Championship ambapo kati ya hiyo kimeshinda minne, sare mitatu na kupoteza 19, kikishika nafasi ya 14 na pointi zake 15, huku eneo lake la ushambuliaji likifunga mabao 21 na kuruhusu 50.

Related Posts