Msajili wa Baraza la Optometria Sebastiano Millanzi, ameonya baadhi ya wataalam wa optometria wanaojitambulisha kwa cheo cha “Daktari” kuwa ni kinyume cha Sheria namba 23 ya Optometria ya mwaka 2007 Sura ya 23, na kusema kitendo hicho ni kosa na linaweza kumtia mtaalam huyo hatiani.
Bw. Millanzi ameongeza kuwa ikidhibitika kuwa kuna mtaalam anayejitambulisha hivyo upo uwezekano mkubwa wa kuchukuliwa hatua za kisheria pale atakaposababisha madhara kwa jamii.
Bw. Millanzi ametoa kauli hiyo Aprili 12, 2025 kwenye ziara ya usimamizi shirikishi mkoani Kilimanjaro, ambapo alibaini baadhi ya wataalam wa Optometria wamekuwa wakijitangaza kama “Madaktari” kinyume na usajili wao.
Sheria hiyo inaelekeza wazi kuwa wataalam wote wa optometria hapa nchini wanasajiliwa kama wataalam wa optometria kulingana na majukumu yao ya kitaaluma na si vinginevyo.
Millanzi alifafanua kuwa huduma za macho hutolewa na wataalam walio katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza ni Madaktari Bingwa au Madaktari wasaidizi wa Macho kundi la pili ni wataalam wa Optometria na kundi la tatu ni Wauguzi wa Macho.
Ameonya matumizi holela ya cheo cha kitaaluma kwani ni hatari kwa afya ya macho kunakotokana na kuwapotosha wagonjwa na jamii kwa kuwafanya wapate huduma tofauti kulingana na sifa stahiki za mtaalam.
Kwa msingi huo, Millanzi amesisitiza kuwa ni muhimu kwa kila mtaalam wa optometria kuheshimu mipaka ya taaluma yake ikiwemo kujitambulisha kwa taaluma yake muhimu kulingana na usajili na kila mtaalam wa optometria aone fahari kuitwa hivyo.
Msajili Milanzi ametumia fursa hiyo kuwaasa baadhi ya wamiliki wa vituo vya optometria kukamilisha usajili wa vituo vyao kwa wale ambao wamekutwa wakitoa huduma pasipo kuvisajili sambamba na uwasilishaji wa taarifa za wagonjwa wa kila mwezi katika Ofisi ya Mganga Mkuu wa Manispaa.
“Vituo vingi havitumii vitabu vya MTUHA kujaza taarifa za wagonjwa hali inayochangia kwa kiasi kikubwa ukosefu wa taarifa muhimu za wagonjwa hata kuathiri upangaji wa Mipango ya Serikali na kudhorotesha utoaji wa huduma bora za afya ya macho kwa ujumla,” amesema Milanzi.
Millanzi amehitimisha kwa kutoa rai kwa wataalam wote wa huduma ya optometria kushirikiana kwa karibu na Baraza la Optometria ili kuhakikisha taaluma hiyo inalindwa na kuheshimiwa na kuwasihi wananchi kuwa waangalifu wanapochagua sehemu ya kupata huduma hizo kwa kwenda sehemu zilizo sajiliwa kisheria.