Iran. Wakati Serikali ya Iran ikithibitisha kufariki dunia kwa Rais wa nchi hiyo, Ebrahim Raisi kwa ajali ya helkopta juzi, maswali yameibuka kuhusu kifo hicho.
Raisi alikuwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Hossein Amir-Abdollahian ambaye pia amefariki dunia wakati walipokuwa wakirejea kutoka nchi jirani ya Azerbaijan kwenye hafla ya uzinduzi wa bwawa.
Wengine waliokuwamo ndani ya helikopta hiyo ni Gavana wa Mkoa wa Azerbaijan Mashariki, Malek Rahmati wa Iran na mwakilishi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Mkoa wa Azerbaijan Mashariki, Ayatollah Mohammad Ali Ale-Hashem pamoja na walinzi.
Viongozi hao walifariki baada ya ajali hiyo iliyotokea eneo la milimani Jimbo la East Azerbaijan.
Ingawa chanzo hakijatajwa, inaelezwa hali mbaya ya hewa ya ukungu ilikuwa imeenea eneo hilo.
Hata hivyo, vikosi vya uokoaji vilivyopata shida kufika eneo la ajali kutokana na ukungu na mvua, baadaye vilipata mabaki ya helikopta hiyo kando ya mlima.
Mkuu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Iran, Pir Hossein Kolivand, alisema waokoaji walipoona mabaki hayo, walisema hakuna dalili za uhai.
Kiongozi mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei aliwataka Wairani wasiwe na wasiwasi kuhusu uongozi, akisema nchi itaendelea bila usumbufu.
Jana, Serikali ya Iran ilifanya mkutano wa dharura asubuhi huku kiti cha Raisi kikiwa kimeachwa wazi na kufunikwa na kitambaa cheusi.
Kifo cha Raisi kinatarajiwa kusababisha mapambano ya madaraka, huku wagombea mbalimbali wenye tamaa wakijitokeza kushindania nafasi hiyo.
Picha zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha raia wa Iran wakitoka mitaani kuomboleza baada ya tangazo la kifo cha Raisi .
Kiongozi Mkuu Ali Khamenei ametangaza kwamba Taifa litaadhimisha siku tano za maombolezo.
Haijulikani ni lini helikopta ya Raisi ilitengenezwa, lakini Bell 212 imekuwa ikitumika na Serikali mbalimbali duniani kwa zaidi ya miaka 50, ikianza kutumika mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Kupitia kurasa zake za kijamii, Rais Samia Suluhu Hassan alituma salamu za rambirambi kufuatia msiba huo kwa niaba ya Serikali na watu wa Tanzania.
“Napenda kutoa pole zetu za dhati kwa Serikali na Watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kifo cha kusikitisha cha Mheshimiwa Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tunaungana nanyi katika kuomboleza msiba wa kiongozi wenu, tunawatakia nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.”
Licha ya Serikali ya Israel kutotoa taarifa rasmi, baadhi ya maofisa wake waliozungumza na Shirika la Habari la Reuters wametangaza kwamba nchi hiyo haihusiki na ajali mbaya ya helikopta iliyosababisha kifo cha Rais Raisi jana.
Israel imekuwa kwenye msuguano na Iran; na hivi karibuni ilishambulia ubalozi wa nchi hiyo nchini Syria na kusababisha vifo vya maofisa wa ubalozi huo.
Hata hivyo, Iran ilijibu kwa kurusha mabomu nchini Israel.
Iran imekuwa ikiliunga mkono Kundi la Hamas linaloendelea na vita na Israel.
Maofisa wa Israel waliotaka majina yao yasitajwe walikataa madai kwamba Tel Aviv ilikuwa nyuma ya ajali hiyo, wakisema: “Haikuwa sisi.”
Kuhusu hilo, Profesa wa historia nchini Tanzania, Abdul Sherif akizungumza na gazeti hili alisema tuhuma za Israel kuhusika na ajali hiyo zinatokana na hila zake za kupanua vita kati yake na Palestina na Kundi la Hamas.
“Israel imekuwa ikipambana kutanua vita yake na Hamas ifike Iran ili Marekani ipate nafasi ya kuingia,” alisema Sherif.
Hata hivyo, alisema suala la hali mbaya ya hewa linaweza kuwa sababu nyingine ya mawingu na ukungu uliokuwa umefunika eneo hilo.
“Kumekuwa pia na mvutano ndani ya Iran, lakini hii dhana imekuwa ikitumiwa na vyombo vya habari vya Magharibi kuonyesha kuwepo kwa mvutano unaoweza kusababisha kifo hicho, japo ni kweli kuna mvutano na hakuna nchi duniani isiyo ma migogoro,” alisema.
Kwa mujibu wa Katiba ya Iran, iwapo Rais atafariki dunia akiwa madarakani, kifungu cha 131 kinasema makamu wa kwanza wa Rais ndiye atakayeshika madaraka, huku baraza linalojumuisha makamu wa kwanza wa Rais, Spika wa Bunge na mkuu wa Mahakama lazima lipange uchaguzi wa Rais mpya ndani ya muda usiozidi siku 50.
Wakati taratibu za mazishi ya Rais wa Iran, Raisi zikiendelea, Makamu wa Rais Mohammad Mokhber anayetarajiwa kurithi nafasi hiyo kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, ameongoza mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Mokhber aliyezaliwa Septemba 1, 1955, anaonekana kuwa karibu na Kiongozi Mkuu Ali Khamenei, ambaye ana kauli ya mwisho katika masuala yote ya Serikali.
Mokhber alikuwa makamu wa kwanza wa Rais mwaka 2021 wakati Raisi alipochaguliwa kuwa Rais.
Mokhber alikuwa sehemu ya timu ya maofisa wa Iran waliotembelea Moscow Oktoba, 2023 na walikubaliana kusambaza makombora ya ardhini na droni zaidi kwa Jeshi la Russia.
Timu hiyo pia ilijumuisha maofisa wawili wakuu kutoka kwa walinzi wa mapinduzi ya Iran na ofisa kutoka Baraza Kuu la Usalama wa Taifa.
Mokhber hapo awali alikuwa mkuu wa mfuko wa uwekezaji unaohusishwa na kiongozi mkuu (Setad).
Mnamo mwaka 2010, Umoja wa Ulaya ulimjumuisha Mokhber kwenye orodha ya watu na mashirika yanayowekewa vikwazo kwa madai ya kuhusika katika “shughuli za nyuklia au za makombora ya ballistic.”
Miaka miwili baadaye, walimwondoa kwenye orodha hiyo.
Mnamo mwaka 2013, Idara ya Hazina ya Marekani iliongeza Setad na kampuni 37 ambazo ilizisimamia kwenye orodha ya mashirika yaliyowekewa vikwazo.
Setad, jina lake kamili ni Setad Ejraiye Farmane Hazrate Emam, au Makao Makuu ya Kutekeleza Amri ya Imamu, ilianzishwa chini ya amri iliyotolewa na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu, mtangulizi wa Khamenei, Ayatollah Ruhollah Khomeini.
Ilielekeza wasaidizi kuuza na kusimamia mali zinazodaiwa kutelekezwa katika miaka ya machafuko baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 na kuelekeza sehemu kubwa ya mapato hayo kwa misaada.
Raisi, ambaye alikuwa Rais wa Iran kuanzia mwaka 2021, alionekana kama mtiifu kwa utawala na mfuasi wa Kiongozi Mkuu Ali Khamenei.
Katika uchaguzi huo, chini ya nusu ya wapigakura wa Iran walijitokeza kupigakura baada ya wagombea wengi wa kati kuzuiwa kugombea.
Alizaliwa Desemba 14, 1960, Mashhad karibu na Jolfa nchini Iran, Raisi alikuwa kiongozi wa kidini wa Iran, mwendesha mashtaka na mwanasiasa aliyewahi kuwa mkuu wa Mahakama ya Iran (2019–21) na baadaye rais wa nchi hiyo (2021–24).
Kama mwanafunzi mchanga katika seminari ya kidini katika mji mtakatifu wa Qom, Raisi alishiriki katika maandamano dhidi ya Shah aliyeungwa mkono na Magharibi katika mapinduzi ya 1979.
Uhusiano wake na viongozi wa kidini huko Qom ulifanya awe mtu anayeaminika katika mfumo wa Mahakama na alikuwa naibu mwendesha mashtaka wa Iran akiwa na umri wa miaka 25 tu.
Raisi alijipandisha haraka hadi nafasi ya juu na kwa kufanya hivyo alipata jina la utani ‘Mchinjaji wa Tehran.’
Kama naibu mwendesha mashtaka na baadaye mwendesha mashtaka mkuu, Raisi alikuwa sehemu ya kile kinachoitwa ‘kamati ya kifo’ ya kundi la majaji wanne waliokuwa wakiongoza Mahakama mwaka 1988 ‘kuwahukumu tena’ wafungwa wa kisiasa wa utawala.
Maelfu ya wafungwa hawa waliuawa kikatili na kutupwa kwenye makaburi yasiyojulikana. Idadi kamili ya vifo haijulikani lakini makundi ya haki za binadamu yanakadiria takriban watu 5,000 waliuawa kufuatia hukumu kali ya Raisi.
Raisi hakuwa tu mtiifu kwa Jamhuri na Kiongozi wake Mkuu Ruhollah Khomeini, lakini katika miaka ya 1980 alikuza uhusiano wa karibu na Rais wa wakati huo wa Iran, Ali Khamenei.
Khamenei aliendelea kuwa Kiongozi Mkuu wa Iran kufuatia kifo cha Khomeini mwaka 1989, na bila shaka alikuwa na jukumu kubwa katika safari ya Raisi kuelekea urais mwaka 2021.
Baada ya Raisi kuchaguliwa, msimamo wake mkali ulionekana zaidi.
Mwaka 2022, aliamuru utekelezaji mkali zaidi wa ‘sheria ya hijab na usafi’ Iran inayozuia mavazi na tabia za wanawake.
Ilikuwa chini ya maagizo haya Mahsa Amini mwenye umri wa miaka 22 alikamatwa Septemba 2022 na ‘polisi wa maadili’ wa Iran kwa kuvaa hijab isiyo sahihi na alikufa siku tatu baadaye hospitalini, jambo ambalo lilisababisha ghasia kubwa.
Miezi ya maandamano ya kitaifa iliyofuata yalikuwa mojawapo ya changamoto kubwa zaidi kwa watawala wa kidini wa Iran tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979.
Mamia ya watu waliuawa, kulingana na makundi ya haki za binadamu, yakiwamo makumi ya maofisa wa usalama waliokuwa sehemu ya ukandamizaji mkali dhidi ya waandamanaji.