Bunda. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ataongoza maziko ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gissima Nyamo- Hanga anayetarajiwa kuzikwa wilayani Bunda Mkoa wa Mara keshokutwa.
Nyamo-Hanga na dereva wake, Muhajiri Haule walifariki dunia kwa ajali ya gari usiku wa kuamkia Jumapili, Aprili 13,2025 baada ya kupata ajali katika eneo la Nyatwali wilayani Bunda mkoani Mara, wakitokea Mwanza kuelekea Bunda.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Aprili 14, 2025 baada ya kukagua maandalizi ya mazishi, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amesema maziko ya Nyamo-Hanga yatafanyika katika eneo la Migungani mjini Bunda, Jumatano Aprili 16, 2025.
Amesema msiba wa Nyamo-Hanga ni pigo kwa Mkoa wa Mara kwa ujumla kwa maelezo kuwa amekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha masuala mbalimbali hususan yahusuyo nishati ya umeme.
“Kama mtakumbuka hivi karibuni tulipata maafa ambapo kaya zaidi ya 300 zilikosa makazi baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo kutokana na mvua iliyonyesha, katika tukio hilo, taasisi nyingi pia ziliathirika ikiwamo Tanesco, lakini nilivyowasiliana na Nyamo-Hanga alihakikisha umeme unarejea ndani ya muda mfupi, niseme Tanesco ilikuwa taasisi ya kwanza kurejesha miundombinu yake kwa ufasaha ndani ya muda mfupi,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Ameongeza kuwa wiki iliyopita pia aliwasiliana na Nyamo-Hanga kuhusu suala la umeme katika hule ya Amali inayojengwa wilayani Butiama, mkurugenzi huyo mtendaji alishughulikia jambo hilo na kulipatia ufumbuzi kwa haraka.
Mwananchi imezungumza na baadhi ya ndugu nyumbani kwa Nyamo-Hanga eneo la Migungani mjini Bunda, wamesema wamepoteza nguzo ya familia huku wakidai hawakuwa na taarifa juu ya ujio wake nyumbani.
Kisyeri Gissima amesema enzi za uhai wake Nyamo-Hanga alikuwa ni mtu mwenye mapenzi na ndugu na jamaa zao na hakuwa mbaguzi bali alikuwa na tabia ya kutembelea ndugu mara kwa mara.
“Mara ya mwisho tulikuwa naye katika Kijiji cha Baranga wilayani Butiama kwenye msiba wa mjomba wake, nakumbuka ilikuwa ni mwezi wa pili mwaka huu na muda wote alikuwa akishirikiana na ndugu bila kujali nafasi aliyokuwa nayo,” amesema Gissima.
Amesema kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo juu ya ndugu na jamaa alikuwa na utaratibu wa kufika mara kwa mara kijijini hapo kuwajulia hali pale wanapopata matatizo yakiwamo ya misiba, licha ya majukumu mengi aliyokuwa nayo.
“Tulishangaa baada ya kupata taarifa za ajali hiyo, sisi kama familia hatukujua kama anakuja huku siku hiyo,” amesema Gissima.
Naye kaka wa marehemu, Robert Nyamo-Hanga amesema;
“Mimi naishi Dar es Salaam, nilipewa taarifa ya msiba na shemeji yangu jana asubuhi, kwa kweli nilipatwa na mshtuko mkubwa na nilipoteza fahamu, ndugu yangu amefariki ghafla mno, nimeumia sana na hakutuambia kama angekuja huku nyumbani, hatuelewi inatuuma sana,” amesema kaka yake huyo.
Robert ambaye anasema ndiye aliyemlea Nyamo-Hanga tangu utotoni, amesema alikuwa ni mtu mwenye upendo wa hali ya juu na msikivu siku zote.
“Kwa kweli alikuwa nguzo ya familia, kifo chake ni pigo kubwa kwetu, mpaka sasa sijui tutafanyaje, nguzo imeanguka alikuwa tegemeo kubwa kwetu,” amesema kaka yake huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amesema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Nyatwali karibu na geti la Ndabaka la kuingia katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Amesema chanzo cha tukio hilo ni dereva wa gari alilokuwamo Nyamo-Hanga aina ya Landcruser kumkwepa mwendesha baiskeli kisha kupoteza mwelekeo na kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa mbele yao.
Lutumo amesema ajali hiyo ilitokea saa 7.30 usiku ambapo baada ya ajali dereva wa lori pamoja na mwendesha baiskeli walikimbia.
Kwa mujibu wa wenyeji wa Wilaya ya Bunda suala la uwepo wa waendesha baiskeli katika eneo hilo kwa muda huo ni jambo la kawaida, na wengi wao ni wauza mkaa.
Joram Sinai amesema wauza mkaa wengi huwa wanafanya biashara hiyo nyakati za usiku ili kuwakwepa maofisa maliasili ambao wamekuwa wakiwakamata wakiwakuta na mkaa.
“Wauza mkaa wengi huwa wanaleta mkaa mjini nyakati za usiku na wanafanya hivyo kuwakwepa watu wa maliasili ambao mara nyingi wanafanya doria usiku na mchana kwa ajili ya wauza mkaa,” amesema Sinai.
Amesema ukwepaji huo unatokana na ukweli kuwa wengi wao hawana vibali vya kufanya biashara hiyo.
Nyambili Gabriel amesema: “Asubuhi wengi wanakuwa shambani au wanapakua mkaa kutoka kwenye tanuru kwa hiyo muda mzuri wa kwenda mjini kuuza mkaa ni usiku,” amesema
Richard Nyoswede amesema hata hivyo pamoja na kuuza nyakati za usiku lakini wauza mkaa hao hawana uhakika wa kufika sokoni na bidhaa zao, kwani mara kadhaa wanakamatwa na maofisa hao ambao pia wameanzisha utaratibu wa kufanya doria usiku.
Mwili wa dereva kuzikwa mkoani Pwani kesho
Mkurugenzi wa Tanesco Kanda ya Ziwa, Satco Nombo amesema mwili wa dereva Muhajiri Haule ulisafirishwa jana kwenda mkoani Pwani kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho.
“Mwili umewasili Pwani tayari na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho na hapa pia maandalizi yanaendelea vizuri, hadi sasa hakuna changamoto yoyote,” amesema