• Benki ya Stanbic Tanzania yazindua “Lipa na Stanbic,” suluhisho la malipo ya kidijitali linalowezesha wafanyabiashara kupokea malipo kutoka kwa mitandao yote ya simu na benki zote moja kwa moja kwenye akaunti zao za benki, kwa haraka, usalama, na hivyo kurahisisha wa ukamilishaji wa mauzo.
• Benki ya Stanbic, ambayo ni ya tatu kwa ukubwa kutokana na faida, inaongeza masuluhisho ya kifedha ya kuboresha njia ya malipo kwa wateja wake.
• Benki ya Stanbic inashirikiana kwa karibu na serikali na wadau wa udhibiti wa sekta ya fedha, ikiwemo kufuata mwongozo wa TANQR uliotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT), ili kuhakikisha suluhisho hili linazingatia viwango vya kitaifa na kuleta mabadiliko chanya katika mfumo wa malipo nchini.
Ijumaa, Tarehe 11 Aprili 2025 | Dar es Salaam, Tanzania – Benki ya Stanbic Tanzania imezindua rasmi huduma mpya ya “Lipa Simpo na Stanbic”, ambayo ni suluhisho la malipo ya kidijitali linalolenga kurahisisha ukusanyaji wa mapato kwa wafanyabiashara nchini. Kupitia mfumo huu wa kisasa wa TANQR, wafanyabiashara sasa wanaweza kupokea malipo moja kwa moja kwenye akaunti zao za benki kwa haraka na kwa usalama zaidi.
Lipa na Stanbic inaweza kutumika katika aina mbalimbali za biashara zikiwemo maduka, super market, vituo vya mafuta, migahawa, maduka ya vifaa vya ujenzi pamoja na watoa huduma wengine—yaani, kwa mfanyabiashara au taasisi yoyote inayotaka kupokea malipo kwa haraka, kwa usalama na moja kwa moja kwenye akaunti ya benki, huku wakiwarahisishia wateja kufanya malipo kutoka mtandao wowote wa simu au benki yoyote.
“Uzinduzi wa leo ni hatua kubwa katika safari yetu ya kuhamasisha mifumo ya malipo ya kidijitali.” alisema Fredrick Max, Afisa Mkuu wa Wateja wa Biashara kutoka Benki ya Stanbic Tanzania, wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. “Tumewasikiliza wateja wetu na kuelewa kuwa wanahitaji njia rahisi, salama, na yenye manufaa zaidi ya kukusanya mapato. Hili ndilo suluhisho lenyewe.”
“Huu ni mwaka wa kipekee kwetu, kwani tunasherehekea miaka 30 ya uwepo wetu nchini. Imekuwa ni safari iliyojaa ustahimilivu, mafanikio, na mchango mkubwa katika kusaidia biashara kuimarika, na hivyo kuchochea ukuaji na maendeleo ya taifa letu kwa ujumla,” aliongeza.
“Kupitia Lipa na Stanbic, wateja wanaweza kupokea malipo kutoka kwa wateja wao kutoka kwenye mitandao yote ya simu pamoja na benki nyingine. Fedha zote huingia moja kwa moja kwenye akaunti za biashara za wateja wetu, jambo linalowezesha usimamizi bora wa mapato na kuboresha usalama wa kifedha wa mteja. Huduma hii ni salama na rahisi, na inarahisisha ukamilishaji wa mauzo kwa kutumia takwimu halisi za biashara.
Huduma hii pia inamsaidia mteja kutengeneza historia ya miamala jambo litakalosaidia wakati anapotaka kuomba mkopo wa biashara kutoka benki yetu. Pia, kwa kutumia Lipa Simpo na Stanbic, wafanyabiashara hawatalazimika tena kutumia mashine nyingi za POS katika sehemu zao za biashara. Stanbic pia imejipanga kuwapatia wateja wake elimu ya kifedha ili kusaidia kuimarisha uendeshaji wa biashara zao,” alisema Sharon Mujuni, Mkuu wa Idara ya Miamala, Benki ya Stanbic Tanzania.
Kwa upande wake, Meneja wa kituo cha mafuta cha Oryx kilichopo Mwenge, Matrona Ngowi alisema, “Hii itakuwa huduma bora kwetu sisi wafanyabiashara ya mafuta kwa Benki ya Stanbic kuturahisishia kwa wateja wetu kulipa kwa kutumia Lipa Simpo na Stanbic ambayo ni huduma ya Lipa namba iliyoboreshwa, malipo yanapofanyika yanaenda moja kwa moja Benki”. Alisema Ngowi.
Afisa Mkuu wa Uendeshaji Tehama Benki ya Stanbic Tanzania, Nelson Swai (katikati) akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya Lipa Simpo na Stanbic ambayo inayotoa suluhisho la kidigitali kwa wafanyabiashara kupokea malipo kwa mitandao ya simu na benki zote nchini. Huduma hiyo ilizinduliwa ijumaa wiki iliyopita. Wengine kwenye picha kulia ni Afisa Mkuu wa Wateja wa Biashara, Fredrick Max na kushoto ni Balozi wa Benki ya Stanbic na Msanii wa Bongo Fleva, Ali Kiba