Mwanza. Wataalamu wa Shirika la Uwakala wa Meli nchini (Tasac) wamewasili jijini Mwanza kuanza uchunguzi wa meli ya Mv Clarias iliyopinduka.
Meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 290 na tani 10 za mizigo, inafanya safari zake kati ya mwalo wa Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza na Kisiwa cha Goziba wilayani Muleba mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Anselm Namala, tukio la meli hiyo kupinduka lilitokea saa 10 alfajiri ya kuamkia Jumapili Mei 19, 2024.
Akizungumza leo Jumanne Mei 20, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa Tasac, Mohamed Salum amesema watalaamu hao aliyowataja kuwa ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya uundaji wa meli na mhandisi mtaalamu wa mitambo ya meli wataanza kwa kufanya mahojiano na watumishi wa meli hiyo.
“Sasa hivi tunahisi huenda meli hiyo ilikunywa maji, ndiyo maana tunatakiwa kufanya uchunguzi wa kitu kimoja baada ya kingine, lazima kuna sababu ndiyo maana tumeleta wataalamu hawa kuangalia nature (asili) lakini sasa hivi tuko kwenye hatua za kukitoa chombo majini,” amesema Salum.
Salum amewatoa hofu wananchi walioshtushwa na tukio hilo huku akisema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji majini ikiwemo kukamilisha ujenzi wa Kituo Kikuu cha Utafutaji na Uokozi ndani ya Ziwa Victoria kinachojengwa eneo la uwanja wa ndege wa Mwanza.
“Serikali inachukua hatua kuhakikisha vyombo vinavyotembea majini vinakuwa salama, tayari tunajenga kituo kikuu cha utafutaji na uokozi Mwanza, Musoma, Sengerema na tunapanga kujenga kituo kingine Kagera. Vituo tunavyojenga tunalenga kuhakikisha vyombo vya majini vinakaguliwa,” amesema.
Alipoulizwa sababu zinazoweza kusababisha meli kupinduka ikiwa imeegeshwa, mtaalamu wa ujenzi wa meli kutoka Tasac, Samwel Chubwa ametaja uwepo wa maji yanayopenya ndani ya meli na kwenye injini kuwa miongoni mwa sababu hizo.
“Meli inatembea juu ya maji kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa wa maji kupenya na kuingia ndani na kusababisha ilale upande mmoja majini, kwa upande wa injini mifumo ya upozaji hutegemea maji kutoka ziwani kwa hiyo inaruhusu maji kupenya, pia valvu zinazotoka kwenye injini kwenda kwenye properer ‘pangaboi’ zinaweza kusababisha maji kupenya.
“Lakini kupata uhalisia wa chanzo cha tukio hilo ndiyo maana tumekuja, tutazungumza na wataalamu waliokuwa wanaiendesha na kuikagua. Tunaamini ikitolewa leo na kupelekwa kwenye cherezo basi kufikia Ijumaa huenda uchunguzi ukawa umekamilika,” amesema Chubwa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Anselm Namala mbali na kusitisha huduma ya usafiri kwenda Kisiwa cha Goziba, tukio la Mv Clarias kupinduka lilikwamisha safari za meli ya Mv Butiama inayotokea Bandari ya Mwanza Kaskazini kwenda Ukerewe mkoani humo.
Alipopigiwa simu leo, Ofisa Uhusiano wa MSCL, Abdulrahman Salim amesema safari za meli ya Mv Butiama inayotoa huduma kati ya Mwanza na kisiwa cha Ukerewe hazijarejea hadi pale Mv Clarias itakaponasuliwa.
“Bado tunaendelea na jitihada za kuinasua na kuiondoa ndani ya maji, tunaamini mara baada ya kufanikiwa kuiondoa basi Mv Butiama itaanza kutoa huduma kwa sababu eneo ilipo Mv Clarias ndipo Mv Butiama inapogeuzia.Tunaomba wananchi wawe wavumilivu tunapambana kutatua changamoto hii,” amesema Salim.
Mkazi wa Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, Yustina Mlola ameiomba Serikali kutumia tukio hilo kama funzo la kuweka vyombo vya kutosha kutoa huduma ya usafirishaji majini ili kutokatisha mawasiliano kati ya wakazi wa maeneo ya visiwani na nchi kavu.
“Kwa mfano, Mv Butiama ambayo ndiyo tulikuwa tunapenda kuitumia kwenda Ukerewe imesitisha huduma kwa sababu ya meli nyingine kupata changamoto, lakini kama kungekuwa na gati linguine kubwa huduma zisingekwama na tusingetumia gharama kubwa kufika tunakokwenda,” amesema Yustina.
Meli ya Mv Clarias ilijengwa na wataalamu kutoka nchini Uingereza mwaka 1961, na imekuwa ikitoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya jiji la Mwanza na Kisiwa cha Goziba wilayani Muleba mkoani Kagera.