BONDIA wa uzito wa juu raia wa Ukraine, Usyk Oleksandr ameandika historia ya kuwa mwanamasumbwi wa kwanza ndani ya karne ya 21 kupata hadhi ya BINGWA ASIYE NA KIFANI (Undisputed) kwenye uzito wake.
Usyk amepata hadhi hiyo baada ya ushindi dhidi ya bondia wa Uingereza, Tyson Fury.
Bingwa asiye na kifani ni bondia anayeshikilia kwa wakati mmoja mikanda ya mashirikisho yote makubwa ya ngumi duniani.
Usyk aliingia kwenye pambano dhidi ya Tyson Fury, alfajiri ya Mei 19 akishikilia mikanda mitatu mikubwa ya WBA, WBO na IBF. Mpinzani wake, Fury alikuwa akishikilia mkanda mmoja wa WBC.
Kwa hiyo ushindi ukamfanya Usyk achukue mkanda wa Fury na kudhibiti mikanda minne kwa wakati mmoja, hivyo kuwa bingwa asiye na kifani. Mara ya mwisho bondia wa uzito wa juu kuwa bingwa asiye na kifani ilikuwa 1999 pale Lennox Lewis wa Uingereza alipomchapa Evander Holyfield na kushikilia mikanda yote.
Mchezo wa ngumi siyo wa ukiritimba, kwamba chama kimoja cha ngumi duniani kishikilie kila kitu kama ulivyo mpira wa miguu.
Kwenye masumbwi kuna vyama mbalimbali vinavyosimamia mchezo huo na vyote vinajitegemea. Ni kama unavyoona Usyk anashikilia mikanda ya mashikirisho manne ya kimataifa. Haya ni mashirikisho huru yanayojitegemea na huendesha shughuli zake bila kubanwa na shirikisho jingine.
Kila mkanda katika hiyo, ni ubingwa wa dunia yaani kama kwenye mpira tungesema Kombe la Dunia. Kwa maana rahisi tungesema Usyk anashikilia makombe manne ya dunia.
Mpira ni mchezo wa ukiritimba sana. Hautaki vyama vingine visimamie mchezo huo kwa namna yao.
TFF, CAF na Fifa hazitaki kabisa na haziko tayari hata kwa bahati mbaya kuruhusu hilo kutokea. Wanataka wasimamie wao tu. Kila nchi, chama ni kimoja tu…na duniani chama ni kimoja tu, basi. Na hao wenye chama wanajiona kama mpira waliutengeneza wao.
Kama kungekuwa na uhuru wa kuwa na vyama vingi vya mpira kama zilivyo ngumi, Tanzania kungekuwa na mashirikisho kadhaa ya mpira. Hii ingesaidia kuzipa timu machaguo ya ligi ya kushiriki. Kama hutaki kushiriki ligi ya TFF, unashirki ligi ya chama kingine na unapata ubingwa wako. Na ukienda kimataifa unachagua mashindano. Kama hutaki mashindano ya CAF, unachagua chama unachotaka.
Hii ingesaidia sana kukuza heshima ya vilabu kwa vyama na ligi zao. Ukitaka nishiriki ligi yako, nipe hela nyingi. Timu zikipata hela nyingi ndivyo zinavyojiimarisha zaidi.
Lakini kwa ukiritimba huu unaoanzia Fifa, klabu hata siku moja haziwezi kuwa na heshima kwa vyama. Ona Real Madrid na harakati za kuanzisha European Super League? Baadhi ya vyama vya nchi kama England na UEFA wenyewe hadi Fifa hawataki.
Cha ajabu, Fifa wanakataa Ulaya kuwa na Super League, lakini wanakubali ligi hiyo iwepo Afrika na rais wake ndiye aliyeileta. Hebu dhania Tanzania kunakuwa na vyama vinne vya kitaifa vya mpira. Kila chama kinaanzisha ligi yake na kinatoa bingwa wake.
Lakini mashindano yanakuwa wazi kwa bingwa wa chama fulani kucheza na bingwa wa chama kingine akimfunga, anampora ubingwa. Kwanza hii ingepunguza sana migogoro. Ukishindwa kufanya kazi na chama fulani, unahamia chama kingine na kufanya nao kazi. Watu fulani wamgeshakuwa na vyama vyao muda huu wanaendesha ligi zao. Lakini viongozi wa mpira hawawezi kuikubali hii, siyo tu Tanzania kwa maaana ya TFF, bali hata Fifa wenyewe.
Matokeo yake timu zinajibembeleza na kujipendekeza kwa vyama vya mpira badala ya vyama kufanya hivyo kwa klabu.
Vyama vya mpira vimelala sana kwa sababu havina presha ya kupoteza wanachama.