Pemba. Mchanga Omar Said, mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 mkazi wa Kijiji cha Sizini Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, anadaiwa kumfukia mtoto wake baada ya kujifungua.
Mwanamke huyo mwenye watoto saba, alitengana na mumewe wake miaka miwili iliyopita, hivyo moja ya sababu ya kufanya ukatili kuogopa aibu kuzaa nje ya ndoa na ugumu wa maisha.
Akizungumza kuhusu tukio hilo leo Jumatatu Mei 20, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Mgeni Khatib Yahya, amesema Mei 18 saa 5: 00 asubuhi alipokea taarifa za mama huyo alijifungua, lakini alichojifungua hakikuonekana.
Hivyo, wananchi walifuatilia kisha kubaini alimfukia mtoto huyo kibandani mwake.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, alimwita mama huyo na kuzungumza naye ambaye alimueleza sababu ya kumfukia mtoto wake mchanga ni hali duni inayomkabili kwani hana mtu wa kumtegemea ndio maana akaamua kuchukua uamuzi mgumu.
“Maamuzi aliyochukua mama huyo sio ya kiutu na ni kitendo cha jinai. Alichokifanya ni ukatili unaoangukia chini ya sheria ya mauaji, kwa hiyo Serikali itamchukulia hatua stahiki kwa kitendo hicho,” amesema Mgeni.
Hata hivyo, amesema mama huyo alihofia kupata aibu kwa jamaa na marafiki kwa kujifungua mtoto huyo nje ya ndoa.
Amesema mama huyo hakupaswa kufanya kitengo hicho badala yake angeripoti ofisini kwake kuangalia namna ya kumsaidia lakini hakufanya jambo hilo.
Daktari wa Hospital ya Micheweni, Daud Rashid Mkasha, amesema walipofika eneo la tukio waliona eneo lililochimbwa na kufukiwa, wakafukua na kukuta mwili wa mtoto ukiwa tayari umeshaharibika.
“Tulifika kwenye tukio hilo tukaona kwenye jiko lake kafukia kisha juu kaweka kuni tukafukua tukakuta mtoto kashaharibika, tukaona mifupa hali hiyo imetuhuzunisha sana kuona kichanga kimepoteza maisha,’’alisema.
Suleiman Shaame Hamad, ni Sheha wa Sizini amekiri kutokea kwa tukio hilo na kushangazwa kitendo cha mama huyo kuchukua hatua ya kukifukia kichanga kisichokuwa na hatia.