Tanzania inavyohitaji mfumo wa elimu mviringo

Nimewahi kuzungumzia jinsi mababu zetu walivyowalea watoto na wajukuu zao ili waelewe kwamba ulimwengu wote una asili ya kuhusiana, kutegemeana, na kuunganika.

Nimekuwa nikiita hii ni falsafa ya mviringo ambao hauna budi kulindwa ili usivunjike au kutenganishwa kwa namna yoyote.

Tuchukue mfano wa gurudumu la baiskeli ambalo ni mviringo. Gurudumu hilo likitoboka au kukatika, baiskeli haitaweza kwenda, na tatizo hilo likitokea katika mwendo mkali mtu anaweza kuumia.

Tumeshuhudia ajali za magari ambapo tairi ikipasuka huleta madhara makubwa. Hivyo mviringo wa tairi ni lazima ulindwe kwa kila hali.

 Mvua isiponyesha viumbe vyote tutaangamia.

 Nilieleza kwamba mababu zetu walielewa vizuri uzito wa kuheshimu, kutunza na kuendeleza mazingira yetu.

Watoto walilelewa katika falsafa hiyo kama tulivyoona juma lililopita.

 Lakini ulipofika hapa kwetu mfumo wa elimu kutoka nchi nyingine zilizotutawala bila hiari yetu, tukashuhudia mfumo wa elimu ambao unagawanya ulimwengu vipande vipande, ati kwa lengo la kupata maarifa mbalimbali.

Tumeona na tunaendelea kuwa na mfumo wa elimu unaogawanya ulimwengu katika masomo kama haya: dini, hisabati, lugha, historia, jiografia, fizikia, elimu viumbe, kemia, uchumi, siasa na kadhalika.

 Mwalimu anaingia darasani anafundisha historia, anakuja mwingine anafundisha jiografia, na mwingine historia, kama vile haya maarifa hayana uhusiano wa kimsingi.

Nimepitia mfumo huo wa elimu na mpaka sasa tunaendelea nao.

 Shida kubwa hapa ni kwamba mwalimu na mwanafunzi hawaoni muunganiko ambao upo katika masomo haya.

Mfumo huu mbovu wa elimu unashindwa kumwonyesha mwanafunzi kwamba kila kitu ulimwenguni kinahusiana na vingine, kinategemea vingine, na kumeungana na vingine (interrelated, interdependent and interconnected).

Madhara ya mfumo huu wa elimu yameonekana duniani mara nyingi. Mwaka 2008 dunia ilishuhudia anguko la uchumu lililotikisa dunia nzima.

Kwa mfano huko Marekani, viongozi wao wa uchumi walikuwa wamepata elimu hiyo katika vyuo vikuu mashuhuri lakini kumbe elimu hiyo haikuweza kuunganisha akili zao na mioyo yao.

Elimu hiyo ilishindwa kuwaonyesha kwamba upo uhusiano wa kimsingi kati ya maarifa na busara.

Busara hukuzwa katika mfumo wa elimu ambao unasisitiza umuhumu wa elimu mviringo, ambayo pia hukuza busara na hekima.  Anguko la uchumi   wa  dunia wa  2008 ulisababishwa na kukosa busara na hekima.

 Kuna msemo katika falsafa ya Wamarekani wa Asili (Native Americans) usemao: Ni mtu kichaa tu anafikiri kwa kichwa chake.

Maana yake ni kwamba mtu akifikiri tu na akili yake, bila kuhusisha moyo wake, matokeo yake ni ukichaa. Hii ni kusema kwamba elimu ambayo inatenganisha viumbe vipande vipande, ambayo haihusishi moyo, huleta majanga makubwa kama tuonavyo duniani sasa.

 Mifano ni mingi: Gaza, Ukraine, Sudan, Sudan Kusini, Demokrasia ya Kongo, umaskini katika nchi zote, na kadhalika. Tunatumia akili kutengeneza silaha za vita, lakini busara haipo kutuonyesha maangamizi ya silaha hizo kwa wanadamu na mazingira yetu.

Hivyo msemo huu ni sahihi: ni mtu kichaa tu hufikiri na akili yake, akasahau kufikiri pia na moyo wake.

 Sasa hivi nafundisha somo mtandaoni (online teaching and learning) linaloitwa:

Matatizo na hoja mbalimbali katika uadilifu zama hizi, (Problems and Issues in Contemporary Ethics). Mmoja wa wanafunzi wangu akasema katika majadiliano darasani: dunia hii ina kichaa. Nakubaliana naye. Tunafikiri na akili tu, mioyo haipo.

Katika mazingira kama haya, wapo wanaopendekeza kwamba tutoe elimu ambayo itaonyesha kwamba ulimwenguni humu kuna uhusiano wa kimsingi, tunategemeana na tumeungana kama kitu kimoja.

Hawa wanapendekeza tuwe na mfumo wa elimu unaoonyesha muunganiko wa masomo kama ifuatavyo:

 Kwanza: masomo yafundishwe kama yalivyo sasa lakini mwalimu aonyeshe uhusiano katika masomo hayo (multidisciplinary education).

 Kwa mfano: Mwalimu aonyeshe uhusiano kati ya elimu viumbe, fizikia, kemia na mazingira, au aonyeshe uhusiano uliopo kati ya jiografia na mazingira, au aonyeshe uhusiano uliopo kati ya siasa, historia na uchumi, na zaidi sana aonyeshe uhusiano uliopo kati ya kila somo, uadilifu na busara.

Mwanafalsafa wa Kiyunani Plato (428-348 B.C.) anasema: Uadilifu ni sehemu nyeti ya kila kitu, kila tulisemalo, tulifundishalo na tujifunzalo. Na hapa inaonekana wazi maana ya kufikiri kwa akili na kwa moyo.

Kwa mantiki hii kufundisha somo lo lote bila kuingiza moyo ndani yake ni ukichaa kabisa.

 Pili, masomo yafundishwe hivyo kwamba mada fulani inazungumzwa kutokana na mitazamo mbalimbali (interdisciplinary education).

Kwa mfano: mwalimu achukue hoja ya umaskini, kisha aizungumzie kutokana na elimu ya historia, siasa, mazingira, uchumi na kadhalika. Hapa wanafunzi wataona uhusiano uliopo kati ya utunzaji wa mazingira, utawala bora, siasa safi na historia.

Tatu, masomo yafundishwe hivyo kwamba mkazo upo kwenye uzoefu wa watu kuliko kwenye somo hili au lile (transdisciplinary education). Mkazo hapa ni maisha kwa ujumla kwa kutumia elimu ya masomo yaliyopangwa.

Lengo hapa ni kumpa mwanafunzi elimu au falsafa ya mviringo, na si kumpa elimu vipande vipande. Mwanafunzi huyu atajengewa uwezo wa kuona ulimwengu uliohusiana, unaotegemeana, ulioungana.

 Mfumo huu wa elimu umejaribiwa katika shule za sekondari kadhaa za marekani na matokeo yake yaliwashangaza wengi.

Wahitimu wa elimu hii wamekuwa na utu zaidi, ni watu wanaojali masilahi ya wengine na ubora wa mazingira, wanafunzi ambao wanafikiri kwa akili na kwa moyo pia.

Mwanafalsafa Socrates (470-399 B.C.) alikuwa mwalimu tofauti sana na walimu wa zama hizi.

Yeye aliwachukua wanafunzi wake wakatoka nje ya darasa na kutembea mitaani na vijijini. Huko aliwaonyesha mazingira wanamoishi, aliwaonyesha faida za vichaka na misitu, aliwaonyesha jinsi mazingira yalinayoathiri uchumu na maisha kwa ujumla.

Aliwaonyesha mubashara uhusiano uliopo kati ya uongozi bora na barabara zao, na kinyume chake pia. Katika kufundisha wanafunzi nje ya darasa na kutumia dunia kama darasa na chanzo cha majadiliano.

Socrates alifaulu kuwafanya wahitimu wake kuwa wabunifu, watu wanaotafakari kwa kina, na wenye busara. Si ajabu kwamba alihukumiwa adhabu ya kifo kwa sababu hiyo.

Related Posts