Serikali kupitia Ofisi ya Rais-Tamisemi imetangaza fursa ya mwezi mmoja kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2024 kubadili tahasusi au kozi wanazosomea sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma mapema mwezi huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alisema hatua hiyo inatoa fursa kwa wanafunzi kubadilisha machaguo ya tahasusi ili kutimiza ndoto za maisha yao ya baadaye.
“Tamisemi inatoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya sekondari mwaka 2024 kubadili machaguo yao ili kutoa nafasi zaidi kwa mwanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalamu stahiki katika maisha yake ya baadaye,” alisema na kuongeza:
“Napenda kuwasihi wazazi na walezi kushauriana kikamilifu na watoto wao na kupata ushauri wa kitaalamu na kabla ya kufanya machaguo sahihi ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao.”
Kama alivyosema Mchengerwa, wanafunzi hawapaswi kukurupuka kutumia fursa hiyo, bali umakini wa hali ya juu unahitajika, kwa kuwa hii ndio hatua muhimu inayojenga msingi wa taaluma ya mtu baadaye.
Mwananchi linajaribu kuangazia nukta muhimu za kuzingatia kwa wanafunzi wanaotaka kubadili tahasusi na kozi, mchakato ambao Serikali inasema utakamilika Aprili 30.
Hatua ya kwanza: Kila mwanadamu ana mapenzi na utashi binafsi, ili kufanikiwa katika hili hatuna budi kuwa na malengo kama binadamu. Katika hatua hii, zungumza na moyo wako, fikiri kile unachokipenda rohoni.
Hatua ya pili: Chagua unachokitaka kwa kuwa ndivyo utashi na mapenzi yako yanavyokuelekeza. Si vibaya kama utakuwa na orodha ya vile unavyovitamani kama fani zako za baadaye. Kumbuka kuipanga orodha hii kwa vipaumbele, kiweke mwanzoni kile unachokitamani zaidi.
Hii ndiyo hatua ya kuusikiliza moyo wako. Fani zipo nyingi kama tutakavyoziona baadaye. Moyo unasemaje, je, unataka kuwa mhasibu, mwanasheria au mwalimu? Orodhesha fani zote unazozitamani katika nafsi yako.
Hatua ya tatu: Jifunze undani wa kila chaguo kwa kusoma, kufuatilia taarifa zake au kwa kuzungumza na watu. Kuna faida nyingi za kuujua undani wa fani uipendayo ikiwamo kujua kama fani hiyo inalipa kimaisha ama la. Pia kupata maarifa ya msingi kuhusu fani fulani kutakuwezesha kujua ni kwa namna gani unaweza kujiajiri au kuajiriwa.
Hatua ya nne: Linganisha nguvu na udhaifu wako kwa kila chaguo. Kumbuka unaweza ukakipenda kitu lakini kikakushinda kwa sababu ya hulka, tabia au hali yako kama mwanadamu. Kwa mfano huwezi kutamani kuwa mtangazaji wa redio au televisheni ilhali una tatizo la kigugumizi.
Hatua ya tano: Ukifika hapa unaweza sasa kufanya uamuzi wa mwisho kwa kuchagua fani uipendayo, inaweza ikawa moja au fani kadhaa ulizozipanga kwa kufuata vipaumbele.
Hatua ya sita: Sasa weka mikakati ya kulifikia chaguo lako. Kwa wewe mwanafunzi, hii ndio hatua ya kuchagua masomo yanayorandana na kile unachokitamani.
Kufanikiwa katika mchakato huu wa kujua fani yako unalazimika kuwashirikisha watu kadhaa muhimu wakiwemo walimu, wazazi, wana fani wenzako, marafiki wanaokujua vizuri na hata watu wengine wenye uelewa wa mambo.
Tafuta fani unayoitaka kwa kuzingatia uwezo wako wa akili kumudu mikikimikiki ya usomaji wake. Acha papara na usifuate mkumbo katika kuchagua fani ili usije kujuta baadaye. Waone waliomo katika fani uitakayo wakueleze uzuri, ubaya wake na hata jinsi ya kupata mafanikio uyatakayo.
Tanzania bado tupo nyuma kwa mambo mengi, nina uhakika hata wataalamu waliobobea katika kutoa ushauri nasaha kuhusu uchaguzi wa fani ama hawapo au wapo wachache mno.
Mtafutaji hachoki, jaribu kutafuta asasi, kampuni ama watu binafsi wanaotoa huduma hizi huku ukikumbuka kuwa huduma hiyo nayo ni bidhaa iliyo sokoni kwa sasa. Jiandae kuingiza mkono mfukoni.
Fuatilia taarifa za watu waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali na soma machapisho kukuza uelewa wa mambo. Ndani ya vitabu kuna utajiri ambao Watanzania wengi tunaukosa kwa kuwa hatuna utamaduni wa kusoma vitabu na majarida. Kuza fikra kuhusu maisha kwa kusoma majarida. Jaribu leo njia hii utayaona matunda yake.
Kuna vitabu maalum kuhusu uchaguzi wa fani, sina ufahamu wa kutosha na vitabu vya Kiswahili lakini kwa wanaoijua lugha ya Kingereza wanaweza kukitafuta kitabu kiitwacho A Structured Guide to Career Selection kilichoandikwa na James O ‘Sullivan
Kwa wajuzi wa mitandao ya kompyuta wana fursa nzuri ya kupitia tovuti zinazozungumzia kwa kina kuhusu chaguzi za fani mbalimbali. Tovuti kama www.collegegrad.com ni maarufu katika uwanja huu.
Umefikiria fani zifuatazo?
Kuna fani ambazo ni muhimu kwa mazingira ya Tanzania na hata yale ya kimataifa. Baadhi ya fani hizi ni kama Tehama na matawi yake, Sheria, Udaktari, Uandishi wa habari, Ualimu, Uhandisi, Biashara, Ufundi, Ukutubi, Utalii, Ukalimani, Fasihi, Utunzi wa vitabu, Ushauri nasaha
Ieleweke kuwa hizi ni fani kwa ujumla wake, bado kila fani ina maeneo maalum zaidi unayoweza kuamua kujikita. Kwa mfano, ndani ya masomo ya biashara unaweza kukumbana na fani ndogo kama uhasibu, masoko, uboharia, uongozi wa biashara na fani nyinginezo.
Kwa wanaoutamani uandishi wa habari, unajua kama mgawanyiko wake ni mkubwa? Jiulize unataka kuwa nani kwa kuwa upo uandishi wa habari za magazeti, uandishi wa habari za redio, televisheni, kuna utangazaji, kuna uandishi wa tovuti, blogu na maeneo mengine.
Vivyo hivyo katika Tehama ambayo ina matawi mengi kama mawasiliano, kompyuta, utengenezaji wa mifumo ya kompyuta, usalama wa mifumo, data na mengineyo.
Hujachelewa huu ndio wakati mwafaka, chagua fani ya maisha uipendayo.