Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa hakutakuwa na sekta itakayokosa fedha kwa sababu ya mabadiliko ya sera ya baadhi ya mataifa zinazolenga kupunguza kuyasaidia mataifa yanayoendelea ikiwemo Tanzania.
Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akijibu hoja za wabunge zilizojitokeza katika Bunge la Kumi na mbili, mkutano wa 19 katika kikao cha sita.
Alisema Serikali imefanya tathmini katika sekta zote kupitia Timu iliyochini ya Waziri Mkuu na kuanza kuchukua hatua baada ya baadhi ya mataifa kubadili sera zao ili kupunguza fedha kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania.
“Tulikuwa na mahitaji ya takribani shilingi bilioni 220 kwenye sekta ya Afya ili kuziba pengo la fedha ambazo tulikuwa tunazitarajia kutoka kwa wadau wa maendeleo, Serikali tayari imetoa kiasi cha shilingi bilioni 98 kwenda kwenye sekta ya afya ili kufidia pengo lililojitokeza na tathmini hiyo inaendelea katika maeneo mengine na utoaji wa fedha utaendelea katika maeneo mengine ambayo yanahitaji fedha”, alisema Dkt. Nchemba.
Aidha, Dkt. Nchemba alimpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuwa ameweza kuivusha nchi kipindi ambacho dunia nzima imekuwa ikipita kwenye msukosuko ya kiuchumi ambayo imekuwa ikitokea mfululizo kwa kipindi cha miaka minne.
Alisema kuwa kulitokea changamoto ya Uviko 19, uhaba wa fedha za kigeni na sasa sera za nje za baadhi ya mataifa ambazo tayari Serikali imeanza kuchukua hatua na kama taifa linaamini litavuka.
Dkt. Nchemba alisema kuwa sekta ya Afya ndiyo iliyoguswa zaidi ambapo Serikali itaendelea kuchukua hatua zaidi ikiwemo kuwekeza fedha kwenye uzalishaji ndani ya nchi wa madawa na vifaa tiba vilivyokuwa vinapatikana kupitia wabia.
Alisema kuwa Mpango wa Maendeleo na Bajeti itakayosomwa katika Bunge linaloendelea, sehemu ya fedha itaelekezwa kwenye viwanda vinavyozalisha madawa ndani ya nchi ili kuweza kujitegemea kama nchi katika eneo hilo.
“Nchi yetu na umri wake na uwezo wake na uwekezaji uliofanyika kwenye sekta ya afya tunaweza kujitegemea kumaliza ugonjwa wa Malaria, magonjwa ya TB, vitenganishi na madawa mengine”, alieleza Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa fedha zingine zitaelekezwa kwenye Bima ya Afya kwa wote kama ambavyo Mhe. Rais alivyotoa maelekezo.
Dkt. Nchemba alisema Serikali itatengeneza mkakati wa kubana matumizi kwenye maeneo yenye uhitaji mdogo na kupeleka fedha kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa na ya lazima kama miundombinu, afya, elimu, maji, umeme na sekta zingine za uzalishaji.
Aidha, alibainisha kuwa Tanzania imeingia kwenye kumbukumbu ya kupanga jambo kubwa na kulitekeleza kama mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambao hata baadhi ya mataifa makubwa hawana mradi kama huo ambao kwa sasa zaidi ya kilomita 722 zinaonekana na sehemu kubwa imeanza kufanya kazi hususani kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma.
Alisema vipande vilivyosalia tayari vina Wakandarasi na upatikanaji wa fedha upo katika hatua za mwisho ambapo kuanzia mwaka wa fedha huu fedha katika vipande hivyo itapatikana ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika.
Aliitaja miradi mingine kuwa ni pamoja na Mradi wa Daraja la Kigongo Busisi ambao umekamilika na sasa upo tayari kwa matumizi na mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Tanga ambapo Tanzania imetekeleza wajibu wake kwa kiasi kikubwa.
Vilevile alisema kuwa tayari amefanya mazungumzo na mawaziri wa kisekta kwenye eneo la barabara, maji, kilimo na sekta nyingine na tayari fedha zimetolewa na na zitaendelea kutolewa
Amesema mambo yote hayo yanahitaji kuongeza mapato, hivyo Serikali imekubaliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza elimu kwa mlipa kodi ili kuweza kulipa kodi kwa hiari kama Mhe. Rais alivyoelekeza ambapo elimu itatolewa kwenye michezo, mashuleni na maeneo mengine.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akijibu hoja za wabunge zilizojitokeza katika Bunge la Kumi na mbili, mkutano wa 19 katika kikao cha sita bungeni jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha)