Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Tabora
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amewaambia Watanzania wakatae kuyumbishwa na vyama vya siasa ambavyo vinahatarisha usalama wa nchi na kusisitiza amani iliyopo si mali ya chama cha siasa bali ni tunu ya Watanzia na lazima ilindwe.
Aidha, amesema ni lazima CCM iwaongoze Watanzania kuilinda amani iliyopo kwa sababu imebeba dhamana kubwa ya kuleta maendeleo huku akiwatahadharisha wanaodhani wanaweza kuitikisa hawawezi kufanikiwa.
Akizungumza katika kikao cha ndani kilichowakutanisha viongozi wa Chama kutoka Wilaya ya Tabora Mjini na Uyui mkoani Tabora, Wasira amezungumzia umuhimu wa Watanzania kutunza amani iliyopo nchini.
“Kuna vyama vya siasa ambavyo vinataka uhuru usiokuwa na mipaka, uhuru usiokuwa na amani hauna maana, na wako wanaotoka kulifanya suala hilo kama mtaji. Tunaposema nchi iko salama maana yake tuko salama kweli na wale wanaodhani tunaweza kutikiswa tunawapa majibu hawawezi kututikisa.
“Sisi Katiba yetu Ibara yake ya tano inasema CCM jukumu lake la msingi ni kushinda uchaguzi, kukamata dola, sasa lazima tukamate dola kwa sababu mapinduzi ambayo tunayaendesha kuleta maisha bora kwa watu hayawezi kupatikana bila sisi kushika dola.
“Kwa hiyo dola ni chombo chetu cha mapinduzi na hatuwezi kukikabidhi kwa chama kingine chombo hiki ambacho hakipo kwa ajili ya wenye vyama ambavyo tumesikia kule Njombe mwenezi aliletewa ‘longolongo’ alipigwa hadi mbavu zikavunjika, tena mwenezi wa kike, alichapwa na wanaume halafu chama cha namna hiyo mkipe dola mmechoka na amani?
“Labda mmechoka na amani maana ukichoka jambo…wanaadamu wanatabia moja ya kuzoea na ukizoea jambo unaweza kuliona la kawaida. Hata hewa unayovuta unaweza kuona hata usipovuta wewe utakuwepo tu, lakini ukweli ikikosekana unakufa.
“Kwa hiyo na amani nayo unaweza kuizoea ukaona hata isipokuwepo wewe utakuwepo, haiwezekani, kajifunze kwa majirani zetu, ikitoweka hairudi. Nenda kaulize maeneo ambayo imetoweka hairudi hata kule ambako hali imetulia visasi vimebaki, visasi vinarithiwa vizazi kwa vizazi, msikubali mkababaishwa na jambo la msingi kuhusu amani yetu,” amesema.
Wasira amewakumbusha wana CCM kuwa chama chochote mtaji wake lazima uwe watu, kuzingatia maadili waliyojiwekea na kusisitiza chama ambacho hakina maadili ni sawa na mkusanyiko watu.
Amesema chama cha siasa lazima kiwe kina kanuni ambazo zinatekelezeka na heshima yake iendelee kuwa mbele hsta ya watu wengine wasiokuwa wanachama.
“Watu wanakitegemea chama chetu, wanaulizana mgombea wa CCM ni nani, hata wasiokuwa wanachama wanataka kujua CCM imemweka nani. Hivyo wanachama wa CCM msiogope na hakuna chama cha kuwasumbua kwa kuwa kuna vyama vya siasa vinafanana na watoto wadogo wanaolia sana kwa mama zao.
“Hata kama hawana sababu, ukimpa maziwa anayamwaga, ukimpa maji anakataa, ukimbeba mgongoni anataka kutoka, sasa mama anachanganyiwa huyu mtoto nimpe nini? Mtoto mtundu na mlalamishi sasa vyama vya namna hiyo haviwezi kutusumbua, sisi ni Chama kikubwa.
“Lakini kwa kuwa navyo vipo mara visaini maadili mara vigome, viseme hapana mara viseme tulikosea kuacha tunataka tena mazungumzo, tunazungumza nini? Vyama vya kutikisa kiberiti vikikuta kiberiti kimejaa wanasema tupunguze njiti.”
Ameongeza CCM inasisitiza kwa viongozi wake nchini nzima waendelee na kazi ya kuwashawishi wanachama na wananchi kukipigia kura katika uchaguzi ifikapo Oktoba mwakq huu na ‘mambo ya Ngoswe wamuachie Ngoswe mwenyewe’.