KINSABE WAISHUKURU RUWASA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI YA BOMBA

Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Peter Bura,akimtua ndoo mama kichwani kama ishara ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan

………………………

Na Daniel Limbe,Chato

WAKAZI wa Kijiji cha Kinsabe kata ya Iparamasa wilayani Chato mkoani Geita wameipongeza mamlaka ya usambazaji maji na Usafi wa Mazingira vijijini (Ruwasa) baada ya kuwanusuru na adha ya kutumia maji ya madimbwi kwa kishirikiana na fisi.

Aidha kijiji hicho hakijawahi kupata maji ya bomba tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika(Tanzania bara) na kwamba kitendawili hicho hatimaye kimeteguliwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Pongezi hizo zimetolewa na Chausiku Bomba(65) mkazi wa kijiji hicho ambaye pamoja na mambo mengine amesema kabla ya Mradi huo walikuwa wakitumia maji machafu huku wakichangia na wanyama wa kufugwa na wale wa polini hali iliyokuwa ikiwasababishia kuugua magonjwa ya matumbo mara kwa mara.

Khadija Khamis, amesema upatikanaji wa maji hayo umesaidia baadhi ya wananchi kuvuta maji ya bomba kwenye makazi yao na kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kijiji jirani kutafuta huduma hiyo jambo lililo saidia kupatikana utulivu wa familia ukilinganisha na awali kabla ya kupatikana huduma ya maji ya bomba.

“Sasa hivi kwa kweli angalau tuna amani katika familia zetu,maana awali watoto wetu walikuwa wanatoka shule na kwenda kutafuta maji, lakini huko njiani wanakutana na vishawishi vya kila aina na wakati mwingine wanatishwa na fisi na kulazimika kurejea nyumbani bila maji” amesema Khadija.

Akielezea utekelezaji wa mradi huo mbele ya mkuu wa wilaya hiyo Meneja wa usambazaji wa maji na Usafi wa Mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya ya Chato, Mhandisi Avitus Exavery, amesema mradi huo wa Kinsabe umekamilika kwa aslimia 98 na kwamba kaya 16 zimevuta maji majumbani huku zaidi ya wakazi 7,040 wanatarajia kunufaika kwa kutumia maji safi na salama.

Amesema mradi huo wa kisima kirefu chenye urefu wa mita 72 una uwezo wa kuzalisha lita za ujazo 12,000 kwa siku na kwamba umetekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 335.2 kwa lengo la kuondoa changamoto za upatikanaji wa maji kwa wananchi wa kijiji cha Kinsabe na vitongoji vya Beda,Kinsabe,Elimu, Nyangugunwa A na Nyangugunwa B.

Kadhalika Mhandisi Exavery amesema kwa kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais Samia zaidi ya bilioni 11 zimetolewa katika kuboresha huduma ya maji wilayani humo, hali iliyosaidia kuongezeka kiwango cha upatikanaji wa maji kwa jamii kutoka aslimia 57 mwaka 2020 hadi kufikia aslimia 72 mwaka 2025.

Kutokana na hali hiyo,Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura, amewataka wananchi kuitumza miradi hiyo ya maji ili iwe endelevu badala ya kuihujumu kwa maslahi ya watu wachache na kwamba jukumu la ulinzi na Usalama ni la kila raia mwema wa Tanzania.

Aidha ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kumtua mama ndoo kichwani,na kwamba hatua hiyo itasaidia jamii kutumia muda mwingi katika uzalishaji mali badala ya kupoteza muda huo kutafuta maji kwa umbali mrefu.

                             Mwisho.



 

Related Posts