Dar es Salaam. Serikali imesema ipo katika hatua ya kuainisha mahitaji, sifa na aina ya teknolojia zinazohitajika katika sekta mbalimbali na kuweka muda maalumu kwa ajili ya kupatikana.
Hatua hiyo kwa mujibu wa Serikali, inalenga kuhakikisha sayansi na teknolojia inapewa kipaumbele katika maendeleo ya rasilimali watu na ubunifu.
Katika utekelezaji wa hilo, vyombo vya habari vimetajwa kuwa mhimili muhimu wa kuelimisha na kuibua habari mbalimbali zenye lengo la kuhamasisha ubunifu.
Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Mei 20, 2024 na Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ladislaus Mnyone katika warsha kwa wahariri na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya 10 ya wiki ya ubunifu iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na Mradi wa Ubunifu wa Funguo chini ya Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) Tanzania.
Amesema maandalizi hayo ya mpango wa Taifa wa teknolojia, utasaidia nchi na wadau kuwekeza katika maeneo ambayo Serikali itakuwa imeyaainisha.
“Hii inafanyika kwa makusudi ili hata haya mabadiliko ya mitalaa na sera yaunganishwe na mahitaji yetu ya nchi katika sayansi na teknolojia,” amesema Profesa Mnyone.
Sambamba na maandalizi ya mpango huo, amesema mkakati mwingine wa kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali watu yenye ubunifu, Serikali inatafuta namna ya kuwatumia Watanzania waliopo nje ya nchi.
“Kwa sasa tunatafuta namna ya kuwatumia diaspora ili wasaidie katika kukuza ubunifu, sayansi na teknolojia. Tunajua wengine wana uraia wa mataifa mengine, lakini tunachokifanya ni kuhakikisha tunawatumia,” amesisitiza.
Mpango mwingine wa kuhakikisha kunakuwa na rasilimali watu yenye ubunifu, amesema kuwatumia wafanyakazi waliopo katika taasisi lakini uwezo wao wa kufikiri ni zaidi ya kazi wanazofanya.
“Kama nchi ni muhimu kuona namna ya kuwatumia watu hao ili kuendana na mahitaji ya sayansi na teknolojia,” amesema Profesa Mnyone.
Kuhusu juhudi za Serikali, Profesa Mnyone amesema mabadiliko ya mfumo wa elimu yamefanyika, rasimu ya mkakati wa matumizi ya Tehama imekamilika na vituo vya umahiri vimeanzishwa kuzalisha wabunifu kuendana na mahitaji ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu amesema ufikiwaji wa malengo hayo, unahitaji mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha, kuibua na kuandika habari zitakazoshawishi umma kuvutiwa na ubunifu.
Katika hotuba yake, Machumu amesema ni muhimu kwanza wanahabari na vyombo vyao viwezeshwe ujuzi na uwezo ili vinaposikia habari kuhusu ubunifu viitazame kwa picha kubwa.
Kadhalika, amesisitiza umuhimu wa kujenga ubobevu kwa wanahabari ambao kimsingi watakuwa na ujuzi na maarifa mapana kuhusu masuala ya ubunifu.
“Katika kulitekeleza hilo, ni muhimu kuwepo wanahabari waliobobea katika habari za masuala ya ubunifu ili inapotokea aina hiyo ya habari waitazame kwa picha kubwa,” amesema Machumu.
Sambamba na hilo, amependekeza kuwepo ushirikiano kati ya vyombo vya habari na asasi za kiraia na wadau wengine na wawezeshe uandishi wa habari za ubunifu kwa wanahabari.
“Kama ni mwelekeo wa Serikali kuna umuhimu wa kutengeneza ushirikiano na vyombo vya habari kwa maana ya kuvielimisha na kuwezesha waandishi wakaripoti habari kuhusu ubunifu,” amesema.
Hata hivyo, Machumu amesema uwezekano wa hayo utatokana na vyombo hivyo vya habari kupewa uhuru wa kutekeleza jukumu hilo.
Ametaka kuwepo mkakati wa mawasiliano utakaohusisha kuwajengea uwezo wanahabari ili wabobee katika uandishi wa habari za ubunifu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji Costech, Dk Amos Nungu amesema pamoja na kuwepo bunifu mbalimbali, zipo zinazoshindikana kuendelezwa kwa sababu ya kukosa soko.
Kwa mujibu wa Dk Nungu, baadhi ya bunifu zinavutia machoni, lakini kiuhalisia hazina soko kwa Tanzania, hivyo kuna haja kwa wabunifu kuzingatia wanabuni kitu chenye walaji.
Meneja wa Mipango wa Mradi wa Funguo chini ya UNDP, Joseph Manirakiza amesema katika wiki hiyo yatashuhudiwa mageuzi ya nguvu katika maendeleo ya ubunifu.
“Baada ya wiki hiyo (ya ubunifu) kuzinduliwa Dar es Salaam, tunatarajia wiki ijayo kwenda Tanga kuhitimisha,” amesema.