Mwanza. Mei 21, 1996 ni siku ambayo dunia iliamshwa na habari mbaya na za kushtua za kuzama kwa meli ya MV Bukoba, ikiwa karibu kuingia ghuba ya Mwanza katika Ziwa Victoria, lakini je, unafahamu nini kilitokea muda mfupi kabla ya meli hiyo kuzama?
Meli hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na Kepteni Jumanne Mwiru ilikuwa ikitokea Bukoka kwenda jijini Mwanza na ilipofika eneo hilo ilianza kuyumba na baadaye kuzama na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 800, lakini simulizi ya Kepteni Mwiru inasemaje?
Katika kesi hiyo ya mauaji namba 22 ya 1998, Kepteni Mwiru na washtakiwa wenzake Gilbert Mokiwa, Alfonce Sambo na Prosper Rugumila, walishtakiwa kuwa Mei 21,1996 saa 1:30 asubuhi, waliwaua watu hao 159 pasipo kukusudia, kinyume cha sheria.
Kepteni Mwiru ndiye alikuwa akiendesha meli kutoka Bukoba kupitia Kemondo Bay hadi Mwanza, Mokiwa alikuwa mkaguzi wa meli, Sambo Ofisa wa Bandari ya Bukoba na Rugumila alikuwa Ofisa wa Bandari ya Kemondo ambako ilipita na kuongeza abiria.
Hata hivyo, mwisho wa kesi hiyo iliyoshuhudiwa mashahidi 32 wakitoa ushahidi wao na vielelezo 15 vya nyaraka vikipokelewa mahakamani, Novemba 29,2002 Jaji Mlay wa Mahakama Kuu aliwaachia huru wote kwa Jamhuri kushindwa kuthibitisha shitaka.
Kepteni Mwiru aliyekuwa mshitakiwa namba moja sasa ni marehemu na Sambo aliyekuwa mshitakiwa namba tatu ambaye naye alifariki muda mfupi baada ya kesi kuanza kusikilizwa na mahakama kuondoa jina lake kuwa miongoni mwa washitakiwa.
Nahodha ashuhudia miili ikielea majini
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, kepteni Cleophas Magoge, aliiambia mahakama siku ajali inatokea alikuwa ofisini jijini Mwanza na saa 2:15 asubuhi na hapo alifika wakala wa abiria kutoka eneo la Kaskazini mwa bandari kwa upande wa Mwanza.
Ambaye alimpa taarifa meli ya MV Bukoba imepinduka na haraka alikwenda upande wa kusini wa bandari kuchukua meli nyingine ya MV Victoria iliyokuwa kwenye matengenezo ya injini na kumtaka Katibu muhtasi ajulishe makao makuu.
Aliichukua meli hiyo na kuiendesha polepole ili kuepuka kuathiri injini yake na alipofika eneo la ajali kwenye aliona meli ya MV Bukoba ikiwa imepinduka juu chini na pia aliona miili ya watu waliokufa na waliookoka wakiwa juu ya maji.
Alipofika, alisema alikuta tayari meli nyingine ya MV Butiama imeshafika na boti zingine na kuongeza kuwa kulikuwa na kuchanganyikiwa kwa vile kila meli, boti na waokoaji katika eneo la ajali walikuwa wanahangaika kuokoa na kuopoa miili
Shahidi huyo aliiambia mahakama wakati huo hakuwa wamepokea maelekezo yoyote kutoka makao makuu ya ofisi yake ya nini afanye kwenye meli na walikuwa hawana vifaa vya kuivuta meli hadi nchi kavu, na wazamiaji wao wawili walikuwa Kigoma.
Akiwa eneo hilo la ajali, Magoge alisikia sauti za watu wakipigapiga meli ya MV Bukoba kwa ndani na hapo alitoa maagizo kutobolewa mashimo kwenye meli ili kuwaokoa watu waliokuwa ndani na kazi ilianza saa 2:30 asubuhi kwa vile iliwalazimu kutafuta gesi.
Katika shimo la kwanza, alisema aliokolewa mtu mmoja tu akiwa hai na aliposikia sauti za watu wakipiga piga kutoka upande mwingine wa meli, aliamuru kutobolewa shimo la pili na kupitia shimo hilo, watu wengine wawili waliokolewa wakiwa hai.
Ni baada ya kutoboa shimo la pili, Kepteni Magoge alisema hewa nyingi ilitoka kwenye meli na ziwa lilikuwa likitengeneza mawimbi makubwa na kutokana na mawimbi hayo, meli ikazama kabisa.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, alipofika eneo la ajali, alimuona nahodha aliyekuwa akiendesha meli hiyo pamoja na mhandisi mkuu wa meli, Adolf Mkude kuwa miongoni mwa watu waliokuwa wameokoka lakini wakiwa bado wako juu ya meli.
Shahidi wa pili, Kepteni Manasse Kombo, aliyekuwa akiendesha meli nyingine ya MV Butiama, alisimulia siku ya tukio saa 2:00 asubuhi, alisikia bandari ya Mwanza kaskazini ikiita MV Bukoba kwa simu ya upepo lakini hakukuwa na majibu.
Mawasiliano hayo yaliendelea huku MV Bukoba ikiitwa pasipo majibu na baadaye ofisi hiyo ilimjulisha shahidi huyo meli ya MV Bukoba ilikuwa haijawasili na hapo alianza kupata mashaka, ambapo naye aliita MV Bukoba mara mbili bila majibu.
Hapo kwa haraka alituma ujumbe wa dharura au hatari kuwa meli ya MV Bukoba imezama na baada ya kutuma ujumbe huo, vituo vingi viliitikia na kutaka taarifa zaidi na hapo aliendesha meli ya MV Butiama kuelekea katika eneo la ajali.
Huko alikuta boti ndogo mbili zikijaribu kuokoa watu wakiogelea, naye aliungana nao na hapo alimuona nahodha wa meli ya MV Bukoba akiwa juu ya meli, na punde ikaja meli ya MV Victoria ambapo watu waliokuwa tayari wameokolewa walipakiwa humo.
Nahodha alivyoamuru spidi ipunguzwe
Shahidi wa 30, Adolf Mkude ambaye alikuwa mhandisi mkuu wa MV Bukoba na aliyekuwepo kwenye meli kuanzia Mei 20, 1996, alisema siku hiyo saa 1:00 asubuhi waliwasili Bukoba wakitokea Kemondo Bay na baadaye ilienda tena Kemondo Bay.
Alikuwa eneo la injini wakati meli ilipotoka Bukoba kwenda Kemondo Bay na wakati meli ikifanya safari zake katika maeneo hayo mawili haikuwa na tatizo lolote.
Hapo ndio ghafla akiwa katika cabin yake, aliona vitu vikirushwa upande mwingine, na kwa haraka alitoka kwenye hicho chumba na kwenda kwenye ukingo wa meli na huko alimkuta Ofisa mkuu akiwa na mabaharia wengine ambapo alimuuliza nini kimetokea.
Kabla hata hajapatiwa jibu, ghafla meli iliyumba kwenda kushoto na nahodha wa meli hiyo (Kepteni Mwiru) naye alifika eneo hilo ambapo alimwamuru msaidizi wake kupunguza spidi ya meli na alimsikia akisema “punguza mwendo, punguza mwendo”
Wakati huo, eneo hilo nalo tayari lilikuwa ndani ya maji na ilipopinduka alijikuta akiwa eneo la juu ya meli na watu wengine akiwamo nahodha na ndipo walipookolewa.
Uwezo wa meli kubeba abiria, mizigo
Shahidi wa 31, Mhandisi Laurent Idudu, alieleza alipangiwa kazi katika meli ya MV Bukoba kuanzia Machi 1996 na hakuwahi kuelezwa meli ina tatizo lolote ingawa alikuwa ameambiwa ilikuwa na tatizo la kutulia (stability problems).
Alieleza uwezo wa meli ya MV Bukoba ilikuwa kubeba abiria 400 na mizigo tani 85 na kipindi chote alichokuwemo wakati ikisafiri kati ya bandari za Mwanza, Port Bell na Kisumu hakukuwa na tatizo lolote na ilipoondoka Bukoba kwenda Mwanza alikuwamo.
Baada ya zamu yake kumalizika alienda kulala na alilala bila kuhisi tatizo lolote la meli hadi saa 2:00 asubuhi alipokwenda chooni ndio aliwasikia abiria wakisema meli imeyumba sana na hapo ndipo iliyumba tena kulia, kushoto kisha kupinduka.
Simulizi za abiria waliokuwamo
Yahaya Rushaka alikuwa miongoni mwa abiria 10 waliotoa ushahidi katika kesi hiyo na katika ushahidi wake alisimulia kuwa walipoondoka Kemondo Bay, meli iliyumba kidogo na alipowauliza wafanyakazi wa Shirika la Reli (TRC), walisema hiyo ni hali ya kawaida.
Alieleza saa 11:00 asubuhi ghafla meli iliyumba hadi friji iliyokuwepo ndani ilianguka pamoja na chupa zilizokuwa mezani, hapo aliogopa sana hivyo akaamua kupanda juu ya meli kwa kuwa kulikuwa na majaketi ya uokozi.
Aliomba na baada ya kumaliza kuomba na kufungua macho aliona watu wakivaa majaketi ya uokozi na wakati huo meli ilikuwa ikiyumba, hapo aliogopa na aliomba apatiwe jaketi la uokozi ambalo alipewa na mmoja wa askari polisi waliokuwepo.
Alieleza meli ilipinduka kati ya saa 1:45 na 2:00 asubuhi ambapo aliona watu wengi na mikungu ya ndizi ikielea na watu wakilia huku wakiomba msaada na aliokolewa saa 5:00 asubuhi na meli ya MV Victoria iliyompeleka meli nyingine.
Kwa upande wake, Zabron Kasindano, alisimulia kuwa siku hiyo ya ajali saa 1:00 asubuhi alisikia habari kuwa meli ilikuwa ikiegemea upande mmoja ambapo kijana mmoja alikuja na kuwaambia wavae majaketi ya uokozi kwa kuwa hali ilikuwa ni mbaya sana.
Alisema hakuvaa jaketi la uokozi kwa kuwa kulikuwa na wanawake eneo hilo waliomcheka huyo kijana wakimwambia ni mwoga, lakini aliamua kupanda hadi eneo la juu ambapo alikuta mikungu ya ndizi ikianguka na kusababisha kelele.
Hapo ndio meli iliyumba kwenda upande mwingine na kupinduka na alijikuta yuko kwenye maji ambapo alitupiwa kamba akaishika na alifanikiwa kupata jaketi la uokozi lililokuwa linaelea na baadaye aliokolewa na wavuvi waliokuwa na meli ya MV Butiama.
Katika hukumu yake baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Mlay aliwaachia huru washitakiwa wote katika kesi hiyo, akisema hakubaliani na ushahidi wa uwepo wa uzembe au meli kutokuwa na uwezo wa kuhimili.
“Katika uchambuzi wa mwisho, hakuna ushahidi wowote wa Jamhuri kwamba abiria walikuwa wamezidi idadi inayotakiwa na kusababisha meli kupinduka. Ushahidi wa Kepteni Kombe wa MV Butiama ni kwamba aliongea na ofisa mkuu wa MV Bukoba.”
“Mazungumzo yake na Eustace sasa marehemu, yalikuwa ni dakika chache kabla meli ya MV Bukoba haijapoteza mawasiliano ya radio na bandari ya Mwanza.
Maneno ya mwisho ya Eustace ni kuwa welcome to Mwanza au Karibu Mwanza,”alisema Jaji.
Ushahidi haukubaliani na nadharia yoyote kuwa kulikuwa na uzembe uliosababisha meli kupinduka ghafla, alisema Jaji Mlay na kuongeza kuwa kilichotokea Mei 21,1996 ni janga lililoshtua, kwa sababu watu wengi walipoteza wapendwa wao na mizigo.
Jaji alisema hata hivyo, majonzi ya watu na Taifa yanaheshimu utawala wa sheria ambao unasema kila mtu hana hatia hata kama kosa ni kubwa kiasi gani, hadi shitaka lake litakapothibitishwa na mahakama baada ya kupima ushahidi wa pande mbili.
Kulingana na Jaji Mlay, ushahidi wa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kuwa mshitakiwa yeyote ana hatia na kwa mifumo ya haki jinai, wanastahili kuachiwa huru kwa makosa yote 159 ya mauaji ya bila kukusudia waliyoshitakiwa nayo.