HISIA ZANGU: Inonga, Simba, siri ya mtungi aijuaye kata

HAUWEZI kuona sana kwa macho, lakini Henock Inonga Baka anavuruga vichwa vya watu wa Simba. Kuna simulizi nyingi nyuma ya pazia, lakini ukweli ni kwamba Inonga anawakoroga Simba ingawa Simba wenyewe wamesimama imara.

Baada ya kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa mtani katika pambano la raundi ya kwanza Uwanja wa Mkapa kuna baadhi ya wachezaji walishutumiwa kuihujumu timu. Ni basi kuna watu ndani ya Simba walitumia busara kwa sababu walikuwa wanakabiliwa na mechi ngumu za kimataifa.

Naambiwa kwamba Inonga ni miongoni mwa wachezaji ambao hawakutazamwa vizuri baada ya pambano lile. Taarifa ya wachezaji kusimamishwa ilisambaa, lakini ikazimwa kwa haraka kwa ajili ya kuendelea kutengeneza mshikamano katika timu.

 Ikaja siku nyingine mbaya kwa Inonga. Ile siku ambayo aliteleza katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro na Samson Mbangula akatumia nafasi hiyo kufunga bao moja kati ya mawili aliyofunga jioni ile. Ni moja kati ya mechi ambayo imefanya watani wachukue ubingwa mapema.

Simba hawakuendelea kutazamana vyema na Inonga. Halafu majuzi katika pambano la marudiano dhidi ya watani, Inonga akachomoka uwanjani mapema na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Kazi ambaye alisababisha penalti kwa Aziz Ki.

Kuna hisia kwa mashabiki kwamba Inonga ‘alijiumiza’ mwenyewe kwa ajili ya kulikacha pambano na kuiacha Simba katika wakati mgumu. Hata pambano hili halijapita hivi hivi. Kuna minon’ongo kutoka kwa watu wa Simba kwamba Inonga aliwauza.

Na sasa ghafla kila kitu kimekwenda haraka kwa Inonga. Kutoka katika jioni ile ambayo alimsindikiza Fiston Mayele wakati anafanyiwa ‘sub’ baada ya yeye na Josh Onyango kumbana vyema mshambuliaji huyo na mashabiki wa Simba kushangilia vilivyo, leo imefika watu wa Simba hawamtazami vizuri. Kumbuka kwamba huyu ndiye mchezaji wa karibuni ambaye mashabiki na mabosi wa Simba walikuwa wamemuweka rohoni. Namna ambavyo watani wao walikuwa wamejaza Wakongomani wengi lakini wao walikuwa na Mcongomani mmoja tu Inonga ambaye alikuwa anacheza kama amekunywa maji ya bendera. Leo kila kitu nasikia kimebadilika.

Nikasikia kwamba mwenyewe ameandika barua ya kuomba kuondoka klabuni hapo. Na naambiwa kwamba hata Simba wenyewe wamepania kuachana naye. Waliridhia ombi lake papo hapo na chochote kinaweza kutokea kuanzia sasa.

Iinchanganya kidogo. Mpira wa Afrika ni mgumu. Simba ina wachezaji wachache mahiri klabuni. Nguzo za kuijenga Simba mpya zinapaswa kuanzia kwa wachezaji wake mahiri wenye uzoefu na ambao wana viwango. Mfano ni hawa kina Inonga, Mohamed Hussein Tshabalala, Fabrice Ngoma, Clatous Chama, Kibu Dennis na wachache wengineo.

Baada ya hapo unaweka wachezaji mahiri kutoka katika usajili mpya ambao umeanza kimya kimya. Tatizo la msingi hapa ni kwamba hata wachezaji ambao wanaonekana watakuwa nguzo za kuanzia nao wapo katika matatizo na klabu.

Inonga ni beki mahiri ambaye alitamba katika michuano ya Afcon akiwa katika kikosi cha DR Congo ambacho mara zote huwa kinasheheni wachezaji ambao wanatamba barani Ulaya. Kama nafasi yake itakwenda kwa Lameck Lawi wa Coastal Union kama inavyosemekana, basi bado kutakuwa na shaka kidogo.

Wachezaji wetu wazawa huwa wanatoka katika klabu zao zilizo katikati ya msimamo wa ligi wakiwa imara. Hata hivyo wakitua Yanga na Simba lolote linaweza kutokea. Ni wachache ambao moja kwa moja wamekwenda kushika nafasi katika timu kubwa kama ilivyotokea kwa mabeki watatu wa Yanga. Bakari Mwamnyeto, Dickon Job na Ibrahim Bacca.

Wengine huwa wanashindwa. Hatuelewi kwa nini. Huwa wanakosa uimara wa akili au presha inakuwa tofauti wanapoingia katika timu kubwa. Mfano ni Waziri Junior ambaye Yanga ilimshinda lakini amerudi tena katika timu ndogo amerudia makali yake.

Kama Simba wamemsajili Lawi hatujui anaweza kuingiaje katika kikosi moja kwa moja. Lakini kuna uhakika na kiwango cha Inonga. Wakipishana moja kwa moja kuna wakati inaweza kuwa hatari. Ni kama Simba walivyotoa washambuliaji wake kina Moses Phiri na Jean Baleke na kuleta wengineo ambao bado wanawafanya mashabiki wagune.

Hata hivyo hatuwezi kuwalaumu Simba moja kwa moja katikati ya hili kwa sababu siri ya mtungi aijuaye ni kata. Labda wao wapo katika nafasi nzuri zaidi ya kukupa ushahidi wa namna ambavyo hawamhitaji tena Inonga kwa sababu ambazo ni wazi hazitakuwa za kiwango chake uwanjani.

Kwa muda mrefu sijawahi kuona wakubwa wetu wakiwa hawana hamu na mchezaji bora, aliye katika mkataba kama inavyotokea kwa Simba na Inonga. Unaweza kuelewa kuhusu Chama kwa sababu mkataba wake unakaribia kukata roho. Lakini lilipokuja suala la Inonga unakuta wazi kwamba huenda kuna kitu kizito zaidi ambacho kimewapa hasira Simba.

Kuanzia sasa mpaka baada ya wiki chache zijazo tunaweza kupata majibu kuhusu suala lake. Kuna wanaodai kwamba FAR Rabat ya Morocco wanamuhitaji. Hauwezi kujua. Kwa kiwango chake cha Afcon ni jambo linalowezekana.

Kama ataondoka zake basi uamuzi wa Simba utapimwa zaidi na kikosi ambacho kitakuja msimu ujao. Kama kikiwa kikali basi mashabiki wanaweza kusahau. Lakini kama kikichwa chepesi mashabiki wanaweza kuwa vigeugeu na kumkumbuka. Bahati hii aliipata Injinia wa Yanga, Hersi Said. Aliwaondoa Djuma Shaaban na Yannick Bangala katika mazingira ya ajabu ajabu, lakini bahati yake ni kwamba amepata mbadala wazuri katika nafasi zao na timu yake inasonga mbele.

Related Posts