Safari  kuhamia Dodoma kukamilika mwakani

Dodoma. Safari ya Serikali kuhamia jijini hapa  itakamilika  baada ya mpango kazi maalumu na ujenzi wa awamu ya pili wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi utakapohitimishwa mwaka 2025.

Aidha, Serikali imesema hadi sasa watumishi wa umma 25,039 wameshahamia huku taasisi zilizohamia zikiwa ni 65.
Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera, Uratibu, Ummy Ndaliananga amesema hayo leo Mei 21,2024 wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Bahi, Keneth Nollo.
Mbunge huyo amehoji ni lini mpango wa   kuhamia Dodoma utakamilika na ni taasisi ngapi zimeshahamia mpaka sasa.
Akijibu swali hilo, Ummy amesema shughuli ya  kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam Kwenda Dodoma lilianza rasmi mwaka 2016. 
Amesema hadi  sasa, jumla ya watumishi 25,039 kutoka Serikali kuu, Bunge, Mahakama, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na taasisi 65 wameshahamia Dodoma.
“Serikali inatarajia kukamilisha mpango wake wa kuhamia Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa kuzingatia mpango kazi maalumu na ujenzi wa awamu ya pili wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi utakaohitimishwa ifikapo mwaka 2025,”amesema.
Katika maswali ya nyongeza, Nollo amehoji ni lini mwisho kabisa wa taasisi za Serikali kuhamia na ujenzi wa makazi rasmi viongozi utaanza lini.
Kuhusu nyumba za viongozi, Ummy amesema kuanzia mwaka 2021/22 kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), walijenga nyumba 20 lakini Septemba 23 mwaka 2023 Makamu wa Rais alizindua nyumba 150.
“Hivi sasa wanapanga  eneo ambalo watalitwaa kwa ajili ya kujenga nyumba za viongozi wa Serikali na watumishi lenye ekari 4,654 katika eneo la Mtumba,”amesema.

Related Posts