Dodoma. Serikali ikishauri wadau kutoa chanjo ya kichaa cha mbwa kupitia sekta binafsi, imetaja mikoa inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama hao.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti ametoa ushauri huo bungeni leo Mei 21, 2024 alipojibu maswali ya mbunge wa Viti Maalumu, Yustina Rahhi.
Katika swali la nyongeza, mbunge huyo amesema ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni changamoto kubwa hasa kwa jamii ya wafugaji waliopo vijijini.
Amesema matibabu yake ni shida kwa sababu hayapatikani katika zahanati na vituo vya afya, hivyo takribani Watanzania 1,500 hupoteza maisha kila mwaka.
Amehoji, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti kichaa cha mbwa.
Mbunge huyo pia amesema namna pekee ya Serikali kudhibiti mbwa wazururaji ni kuwapiga risasi, hivyo kukiuka haki za wanyama.
Amehoji kutokana na idadi kubwa ya mbwa nchi, Serikali haijafikiria kufanya uchumi wa mbwa kwa kuwafundisha na kuwauza ndani na nje ya nchi.
Mnyeti amesema Serikali imeruhusu wadau kutoa chanjo kupitia sekta binafsi.
“Dawa ya kwanza ya kichaa cha mbwa ni kumchanja mbwa mwenyewe, tusisubiri mpaka mbwa augue kichaa cha mbwa ndipo achanjwe kwa sababu anapougua matibabu yake huwa ni muhimu sana,” amesema.
Ametoa rai kwa wadau wote kuendelea kuchanja mbwa ili kudhibiti kichaa cha mbwa kwa sababu hakuna mbadala mwingine tofauti na hapo.
Amesema mkakati wa Serikali ni kuhakikisha mbwa wote nchini wanaendelea kuchanjwa kwa wakati.
Kuhusu mkakati wa kuzuia mbwa wanaozurura mitaani, Mnyeti amesema anapougua kichaa udhibiti wake ni pamoja na kuchukua hatua ngumu kidogo.
Amesema hatua zenyewe ni pamoja na kumuondoa duniani na hakuna mbadala wa kuendelea kuishi na mbwa aliyechanganyikiwa katika hali hiyo.
Amesema Serikali hutoa vibali vya kumuondoa mbwa duniani lakini wapo tayari pia kupokea maoni ya namna ya kufanya.
Akizungumzia idadi ya wanyama hao, Mnyeti amesema Mkoa wa Geita unaongoza kwa kuwa na mbwa 302,879 kati ya milioni 2.77 waliopo nchini.
Amesema taarifa ya sampuli ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2020, ilikadiriwa kuwa na mbwa milioni 2.77 nchini.
Mnyeti amesema kupitia taarifa hiyo mikoa iliyoongoza kwa mbwa wengi mbali ya Geita ni Mwanza yenye mbwa 287,270 na Tabora 243,768.
“Wizara itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kuhakikisha takwimu sahihi za mifugo ikiwemo mbwa zinapatikana kwa wakati ili kuwezesha mipango ya Serikali ya kuendeleza sekta ya mifugo,” amesema.