SERIKALI imewataka waathiriwa wa bomoabomoa ya upanuzi wa barabara ya Morogoro kuanzia Kimara – Kibamba uliofanyika mwaka 2017/2018, kuelewa kwamba Serikali ilitumia sheria ya barabara ya mwaka 1932 na hakuna fidia itakayoweza kulipwa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Imesema kulingana na Sheria hiyo Na. 40 ya mwaka 1932, hifadhi ya barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), ilikuwa ni mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kila upande isipokuwa kwa barabara hiyo ya Morogoro ambayo hifadhi yake ilikuwa kati ya mita 22.5 hadi 121.9 kuanzia Dar es salaam City Hall hadi Daraja la Ruvu.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kibamba, Issa Mtevu (CCM) aliyeitaka Serikali kutoa maelekezo rasmi kwa halmashauri na wananchi ili wasiendelee kufuatilia madai yao kwenye ofisi ya mbunge hasa ikizingatiwa sheria hiyo ndiyo iliyotumika kuvunja makazi yao.
“Ni sheria ya mwaka 1932 ndiyo iliyotumika, hivyo wananchi waelewe kuwa serikali ilitumia hiyo sheria,” amesisitiza Kasekenya.
Majibu hayo ya Serikali yanakuja ikiwa imepita miaka miwili tangu iliposema inasubiri Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itafsiri sheria ya barabara ya mwaka 1932 pamoja na Kanuni zake za mwaka 1955 na marekebisho yake Na. 13 ya mwaka 2009, ili kutambua kama wakazi wa Kimara – Kibamba waliobomolewa nyumba zao walipwe fidia au lah.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu (CCM), ukomo wa kuweka alama za upana wa barabara mpaka Vijijini na kuwataka wananchi kubomoa nyumba kutumia sheria ya mwaka 1932 na 2007.
Kasekenya aliendelea kufafanua kuwa Tanroads imeweka alama ya x ya rangi nyekundu kwa mali za wananchi zilizopo ndani ya mita 22.5 na kuwataka wananchi waondoe mali hizo kwa gharama zao wenyewe kwa kuwa wamevamia eneo la hifadhi ya barabara.
“Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007 iliongeza hifadhi ya barabara zinazosimamiwa na Tanroads kutoka mita 22.5 kuwa mita 30 kutoka katikati ya barabara kila upande. Katika kutekeleza Sheria hii, Tanroads imeweka alama ya x za rangi ya kijani kuonesha eneo la mita 7.5 liliongezeka kila upande ambapo wananchi waliopo katika eneo hili hawapaswi kuondoa mali zao mpaka watakapolipwa fidia,” amesema.