JKU ubingwa inautaka. Vinara wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), JKU imezidi kujiweka pazuri katika kampeni za kubeba ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu huu, baada ya jioni ya jana kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KVZ kwenye Uwanja wa Amaan Kwa Wazee, mjini Unguja.
Maafande hao wa Jeshi la Kujenga Uchumi, ilipata ushindi huo kwa mabao ya dakika za lala salama yaliyowekwa kimiani na Suwedi Juma Hussein na Neva Adelin Kaboma na kuifanya ifikishe ushindi wa 17 kati ya mechi 25 ilizocheza hadi sasa katika ligi hiyo.
Timu hiyo imefikisha pointi 56 na sasa kuhitaji alama 13 tu kati ya 15 kupitia mechi tano ilizonazo mkononi ili kutangaza ubingwa mapema.
Kama JKU itashinda mechi zote tano zilizosalia kufunga msimu itafikisha pointi 71, lakini hata ikivuna alama 13 tu, kupitia mechi hizo itaifanya ifikishe pia pointi 69 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine ikiwamo Zimamoto iliyopo nafasi ya pili na alama 50 baada ya mechi 24.
Zimamoto kama itashinda mechi sita ilizonazo mkononi, itaifanya ifikishe 68 tu, huku watetezi, KMKM inayoshikilia taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo iliyopo nafasi ya tatu kwa sasa ikiwa na pointi 48, iwapo itashinda mechi sita ilizonazo mkononi itafikisha 66 tu, huku KVZ iliyopo Nne Bora ikiwa na pointi 47 ikishinda mechi tano itavuna alama 62.
Katika mechi hiyo, JKU ilitumia dakika tatu za mwisho za pambano hilo kali kupata ushindi huo baada ya awali mashabiki waliohudhuria mchezo huo kuamini ngoma ingeisha kwa suluhu.
Suwedi aliandika bao la kwanza dakika ya 87 na sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho ya mchezo Neva Kaboma aliyesajiliwa na JKU katika dirisha dogo kutoka Kipanga alikwamisha wavuni bao la pili na kuwaduwaza KVZ iliyosalia nafasi ya nne na pointi 47 baada ya mechi 25.
Hilo lilikuwa ni bao la nne kwa nyota huyo katika ligi hiyo kwa msimu huu.
Katika pambano jingine lililochezwa kwenye Uwanja wa Mao A, mjini Unguja Chipukizi ya Pemba iliwabana wenyeji wao Kipanga na kutoka nao sare ya bao 1-1.
Chipukizi ndio iliyokuwa ya kwanza kuandika bao dakika ya 27 kupitia Mansour Saleh Ali kabla ya William John Patrick kuisawazisha Kipanga katika dakika ya 35, likiwa ni bao la pili kwake kwa msimu huu katika ligi hiyo.
Matokeo hayo yamezifanya timu hizo kuongeza alama moja kila moja, lakini zikisalia nafasi ilizokuwapo awali, Chipukizi ikiwa ya sita n pointi 36 na Kipanga ikiwa nyuma yao na alama 35 kila moja ikicheza michezo 24.