Waziri mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak ameahidi kulipa fidia ya paundi bilioni 10 sawa na Sh 32.9 trilioni kwa watu waliowekewa damu yenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na homa ya ini. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Kashfa hiyo imelikumba taifa hilo baada ya uchunguzi wa umma kubainisha kuwa mamlaka ya nchi hiyo iliwaweka waathirika katika hatari isiyokubalika na kuficha maafa makubwa ya matibabu katika Huduma ya Afya ya Taifa katika miaka ya 1970 -1998.
Akihutubia bunge la nchi hiyo jana Jumatatu, Waziri mkuu huyo alisema serikali italipa chochote itakachogharimu kutokana na ripoti juu ya kashfa hiyo, ambayo watu 30,000 wameambukizwa.
Alisema Serikali itatoa maelezo ya fidia leo Jumanne ambapo jumla ya paundi hizo bilioni 10 zimetengwa kama fidia kwa waathiriwa hao.
Uchunguzi wa damu iliyoambukizwa uliwatuhumu madaktari, serikali na Huduma ya Afya ya Taifa kwa kuruhusu wagonjwa wa Hemophilia kuambukizwa virusi vya ukimwi na homa ya ini walipokuwa wakipokea matibabu na kusababisha vifo vya 3,000 hadi sasa.
Hemophilia ni mojawapo ya magonjwa ya kurithi ambapo mwili hukosa uwezo wa kugandisha damu baada ya kupata jeraha kutokana na kukosa au kupungua kwa vigandisha damu. Vigandisha damu ni protini maalumu zinazozalishwa ndani ya mwili.
Wagonjwa hao wa hemophilia huko nchini Uingereza wanadaiwa kupatiwa vijenzi damu vya ugonjwa huo zilizoingizwa kutoka Marekani na kuidhinishwa na mamlaka za Uingereza.
Dawa hizo zinazotengezwa kwa plasma ambayo inatoka kwa watu waliojitolea, inadaiwa kuwa waliojitolea walikuwa ni watu kutoka makundi hatari ikiwamo machangudoa, mashoga na wengine wanaofanya biashara ya ngono.