Gamondi, Aziz Ki waitisha Dodoma Jiji

HAIJAISHA hadi iishe, hivi ndio unaweza kusema baada ya kocha wa Yanga kutangaza vita kwenye mechi tatu zilizobaki ikiwemo ya kesho dhidi ya Dodoma Jiji kuwa hawajakamilisha ratiba na wanataka rekodi.

Kiungo wa timu hiyo, Stephane Aziz Ki ameungana na kauli ya Gamondi akisisitiza kuwa bado wanayo kazi ya kuendelea kuwapa furaha mashabiki wao bila kujali kwamba wametawazwa mabingwa mara 30 wa ligi hiyo msimu huu.

Yanga itakuwa ugenini ikivaana na Dodoma Jiji kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ikiwa tayari imetawazwa bingwa baada ya kufikisha pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote na wenyeji wao wapo katika nafasi ya 11.

Wakizungumza na Mwanaspoti, kwa nyakati tofauti wamesema furaha ya ubingwa inatakiwa kuendana na rekodi nzuri ya kumaliza msimu kwa kushinda michezo mingi na sio kukubali kuwa daraja la timu nyingine kupata matokeo.

“Ni kweli tumeshatawazwa ubingwa bado tunafukuzia rekodi ya kuto kufungwa michezo mingi msimu huu hivyo wapinzani wasitarajie kukutana na mteremko kutoka kwetu bado tunahitaji kushinda michezo iliyobaki,” amesema Gamondi.

“Kutawazwa kuwa mabingwa sio sababu ya kuwatunya tukabweteka bado tunazihitaji pointi nyingine nyingi ili kuwa tofauti na wapinzani wetu ambao wanapambania nafasi ya pili.”

Naye Aziz Ki amesema bado ana kazi ya kuhakikisha timu  yake inamaliza ikiwa inaendeleza rekodi ya kushinda mechi mfululizo sambamba na yeye kufikia lengo la kutwaa kiatu cha dhahabu kwa kufunga zaidi mabao.

“Hatuwezi kuwa daraja la wengine kubaki Ligi Kuu kwa kukubali kufungwa kirahisi tutacheza kwa moyo na ushindani kuhakikisha tunapata matokeo mazuri bila kujali ubingwa tuliotwaa mapema,” amesema.

“Tunatambua uigumu tutakaokutana nao kutoka kwa wapinzani wetu ambao wanapambana kuhakikisha wanajihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao kutokana na kuwa kwenye nafasi mbaya kwenye msimamo.”

Related Posts