Israel yafanya mashambulizi Kaskazini na Kusini mwa Gaza – DW – 21.05.2024

Katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia jeshi la Israel lilitumia matingatinga kuyasambaratisha maduka na majengo mengine karibu na soko katika operesheni inayoendelea iliyoanza wiki mbili zilizopita. Israel inadai kuwa imerejea kwenye kambi hiyo ambako miezi miwili iliyopita ilidai kuwa ililisambaratisha kundi la Hamas.

Hayo yakijiri Wizara ya afya ya Palestina imeripoti kuwa vikosi vya Israel vimewauwa Wapalestina saba baada ya kuuvamia mji wa Jenin katika Ukingo wa magharibi.

Soma zaidi:Mapambano makali yashuhudiwa kusini na kaskazini mwa Gaza

Watu hao wameuwawa wakati jeshi la Israel likisema kuwa limefanya mashambulizi ya anga yaliyolenga maeneo 70 ndani ya saa 24 katika Ukanda wa Gaza.

Mbali na watu saba waliouwawa Jenin, wizara ya afya ya Palestina imesema watu wengine tisa wamejeruhiwa Ramallah na miongoni mwao, wawili wana hali mbaya. Awali jeshi la Israel liltangaza kuwa limeanzisha operesheni ya kupambana na ugaidi mjini Jenin.

Shirika rasmi la habari la Palestina, Wafa, limeripoti kuwa miongoni wa waliouwawa ni daktari bingwa wa upasuaji Usaeed Jabareen, wa hospitali ya serikali mjini Jenin. Limewataja pia mwanafunzi mmoja na mwalimu kuwa ni kati ya waliouwawa.

Vifaru vya Israel vikizunguka Jenin
Vifaru vya Israel mjini JeninPicha: Zain Jaafar/AFP

Mazungumzo ya usitishaji vita kati ya Israel na Hamas yaendelea kusuasua Qatar

Hayo yakijiri, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Qatar Majed Al-Ansari amesema kuwa mazungumzo ya kusitisha vita Gaza na kuwaachilia mateka kati ya Israel na kundi la Hamas yanakaribia kukwama.

Alipoulizwa kuhusu hatua ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kutaka kuwakamata baadhi ya viongozi wa Israel na Hamas, Al Ansari amesema ni mapema mno kwa Qatar kusema chochote. Hata hivyo ameweka wazi kuwa nchi zote na mashirika yanapaswa “kuwajibishwa kwa mauaji ya raia.”

Soma zaidi: Israel, Hamas zapinga waranti wa kukamatwa viongozi wao

Katika hatua nyingine, maafisa wa Israeli wamezikamata kamera za shirika la utangazaji la The Associated Press kusini mwa nchi hiyo. Israel inalituhumu shirika hilo kwa kukiuka sheria mpya za habari kwa kulipa picha shirika la utangazaji la Aljazeera la nchini Qatar.

 

Related Posts