Maadhimisho ya Miaka 60 kati ya Tanzania na China katika sekta za Utalii na Utamaduni yaliyoambatana na Misafara ya Kutangaza Utalii wa Tanzania yamehitimishwa leo Mei 21, 2024 katika Jiji la Guangzhou, China.
Hafla hiyo ya kuhitimisha imehusisha uoneshwaji wa Filamu ya “Amazing Tanzania”kwa mara ya kwanza katika jiji la Guangzhou ambapo watazamaji wengi wa China walionekana kunyanyua simu zao na kupiga picha maeneo mbalimbali yaliyokuwa yakioneshwa au wakipiga makofi.
Akizungumza mara baada ya hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania(TTB) Ephraim Mafuru amesema kwa ujumla misafara hiyo iliyoanzia Bejjing na Shanghai imekuwa yenye mafanikio makubwa kwani pamoja na hamasa ya watalii wengi kuja Tanzania pia wamepata wawekezaji China ambao wako tayari kuwekeza kujenga hoteli ya nyota tano yenye vyumba 100 na wengine walionesha utayari wa kujenga hoteli ya vyumba 50 huku pia kampuni nyingine ikiahidi kuanza kuleta ndege yenye watalii 130 mwezi ujao.
Aidha, kipindi mashuhuri cha televisheni ya Hunan TV kiitwacho “In the Road With the Divas” kinakuja kurekodiwa Tanzania mwaka huu kikiwa na mastaa kadhaa wa China.
Mwananchi mmoja kutoka China aliyejulikana kama Xiaoyang amesema filamu ya “Amazing Tanzania” ni kivutio kikubwa sana kinachoonesha uzuri wa Tanzania.
“Nimependa yale maeneo aliyotembelea Msanii wetu Jin Dong na Rais Samia, ninatamani siku moja nifike Tanzania nami nitembelee maeneo yale yale aliyofika Jin Dong,” alisema Xiaoyang.