Hali bado tete kijiji kilichozungukwa na maji Manyara

Manyara. Hali bado tete kwa wakazi 600 wa Kijiji cha Manyara, Wilayani Babati mkoani Manyara, waliokosa mahali pa kuishi baada ya makazi yao kukumbwa na mafuriko yaliyotokea ziwa Manyara.

Ziwa Manyara limejaa na kutema maji kwenye kijiji hicho na kusababisha watu hao 600 kukosa makazi.

Mmoja ya wakazi wa kijiji hicho, Eliud Hotay akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Mei 21, 2024 amesema japokuwa mvua hazinyeshi, maji yaliyotuama ni mengi na yamejaa kwenye nyumba zao.

Hotay amesema mafuriko yamewakumba baada ya Ziwa Manyara kufurika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha wiki iliyopita kwenye maeneo mbalimbali yanayomwaga maji kwenye ziwa hilo.

“Pia mashamba yetu yamesombwa na maji hayo kwa sasa hatuelewi tutaishi namna gani sisi na familia zetu, hatuna hata vyakula,” amesema Hotay.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Margareth Bomboo amesema wanamshukuru Mungu mvua imesimama kunyesha, na hali ikiendelea hivyo, maji hayo yatazidi kupungua kwenye maeneo mbalimbali.

“Lakini tupo kwenye wakati mgumu kwelikweli watoto wetu walikuwa wanalia kwa hofu na sisi tumepata hasara ila tunashukuru kwa yote yaliyotokea,” amesema Bomboo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Manyara, Juma Jorojik amesema wananchi wa eneo hilo bado wana hali tete kutokana na tukio hilo kwani maji yametuama.

“Wakazi 600 wa kijiji hiki hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kufunikwa na maji yaliyotokana na mafuriko hayo yaliyotokea ziwa Manyara,” amesema Jorojik.

Amesema mashamba yao yakiwa na mazao ikiwemo mahindi, maharage, ufuta na mengine yamefunikwa na maji yaliyotokana na mafuriko hayo.

“Chanzo cha mafuriko hayo ni mvua zinazonyesha kupeleka maji ziwa Manyara na kuingiza kwenye kijiji chetu hivyo kuzua sintofahamu na taharuki,” amesema.

Akitembelea kijiji hicho jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na mbunge wa Babati vijijini, Daniel Sillo alitoa msaada wa magunia 10 ya mahindi kwa waathirika wa mafuriko hayo.

Sillo alisema Serikali itaendelea kutoa msaada ya hali na mali kwa wananchi hao ili kuhakikisha wanakuwa salama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo amewaagiza wataalamu kuendelea kufanya tathmini ya maafa hayo.

Mbogo pia amemtaka Mganga mkuu wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanachukua tahadhari ya magonjwa ya mlipuko yasije kuwakumba wananchi hao.

Related Posts