‘Hakuna uchumi imara bila teknolojia na ubinifu’

 Dar es Salaam.  Serikali imesema hakuna inchi itakayoendelea na kujenga uchumi kama haitawekeza katika teknolojia na ubunifu.

Hayo yamesemwa leo Mei 21, 2024 na Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Corolyne Nombo, wakati akizindua wiki ya ubunifu kwa mwaka 2024 yenye kauli mbiu “Ubunifu kwa uchumi shindani.”

Akizungumza katika uzinduzi wa wiki ya ubunifu iliyondaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia  (Costech) na Mradi wa Ubunifu wa Funguo chini ya Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) Tanzania, Profesa Nombo amesema:“Hakuna nchi itakayoendelea na wala hakuna nchi itakayojenga uchumi wake kama haitawekeza katika teknolojia na ubunifu.

“Kwa hiyo Tanzania imetambua hilo na imeshawekeza kupitia Costech kwa kuwaandaa vijana watakaotengeneza teknolojia na bunifu zitakazowezesha kuingia katika soko la ushindani.”

“Tunatambua umuhimu wa teknolojia ndio maana nchi yetu inawekeza wabunifu kupitia Costech na majukwaa mbalimbali kuhakikisha tunapata wabunifu mahiri ambao watatua changamoto tulizonazo na kufanya nchi yetu iingie katika uchumi shindani, kwa hiyo nchi yetu  imejipanga vizuri.”

“Leo tumefungua wiki ya ubunifu kwa mwaka 2024 jiji hapa, lakini kuanzia Mei 25 hadi Mei 31, 2024 jijini Tanga, tutakuwa na maonyesho makubwa yanayohusiana na masuala ya elimu, ubunifu na sayansi na teknolojia.

“Kupitia Costech tumeweza kuzindua wiki ya ubunifu ambayo imeleta wabunifu mbalimbali kujadiliana masuala muhimu yanayohusiana na ubunifu, nini kinafanya ubunifu uendelee, nini kinafanya ubunifu uwe wa kibiashara, mazingira ya kisera yakoje na mazingira yakibiashara yakoje,” amesema Profesa Nombo.

 Amesema katika wiki ya ubunifu, wamewaasa wabunifu woliopo waendelee kujiongeza, huku Serikali ikitambua umuhimu wao ili kufikia lengo kubwa la maendeleo ya nchi; na kwa sasa Serikali inaandaa dira ya maendeleo ya mwaka 2050.

“Hatuwezi kuendelea bila kuwa na wabunifu, kwa hiyo wabunifu wetu wamepewa muelekeo kule ambako nchi inataka kwenda katika miaka 25 ijayo na kuonyeshwa kwamba bila ubinifu, bila sayansi na teknolojia hatutafika tunapotaka kwenda,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu kundi la watu la wenye ulemavu wanafikiaje kwenye uchumi jumuishi, Profesa Nombo amesema Serikali inatambua makundi yote yaliyopo katika jamii na kuna sera na miongozo inayoelekeza umuhimu wa kumhusisha kila Mtanzania.

“Mimi katika wizara yangu ya elimu, kuna mkakati wa elimu jumishi, hakuna Mtanzania yeyote atakayeachwa nyuma iwe ni kwa kupitia elimu ya kawaida au elimu ya kidijitali, kwa hiyo mkakati huo unatuelekeza namna ya kujumuisha kila Mtanzania bila kujali hali yake kupata elimu bora itakayomsaidia kuwa raia bora,” amesema Nombo.

Amesema teknolojia ndio njia bora katika kusaidia watu wenye mahitaji maalumu kupitia miradi mbalimbali na mipango ya kiserikali.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu  amesema Serikali kupitia tume hiyo imekuwa wadau katika wiki ya ubunifu kwa sababu imeona tija iliyopo.

“Wiki ya ubunifu tunachukua kama mojawapo ya yale mazingira wezeshi ambayo Serikali inatakiwa iyaweke kuhakikisha ubunifu unawezekana,”amesema Dk Nungu.

“Kwa hiyo, wiki ya ubunifu ni jukwaa ambalo limekuwa linawaleta pamoja Serikali, watunga sera, wabunifu wenyewe, washirika wa maendeleo, vyuo vikuu pamoja na mengine, kuonyesha hizi bunifu zetu, lakini pia kujadiliana.”

Amesema wanajivunia wiki ya ubunifu kwa sababu imekuwa ni jukwaa la kuwezesha majadiliano ya ubunifu na wavumbuzi.

Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini, Sergio Valdin amesema kwa miaka 10 sasa wiki ya ubunifu imekuwa ni jukwaa linalowaleta pamoja wabunifu na wavumbuzi kwa lengo la kukuza uchumi na maarifa.

Wiki hiyo ya ubunifu imeandaliwa na Costech wakishirikiana na Funguo kwa udhamini wa Vodacom na kampuni mbalimbali.

Related Posts