Walioua, kuteketeza ndugu wawili kwa petroli wahukumiwa kunyongwa

Moshi. Hivi unajua madhara ya kujichukulia sheria mkononi? Dereva bodaboda Valerian Massawe, amehukumiwa adhabu ya kifo kwa kuwaua kikatili ndugu wawili, waliowatuhumu kuiba pikipiki.

Tukio hilo lilitokea Februari 9, 2022 huko Kibosho Wilaya ya Moshi, kundi la watu liliwakamata ndugu hao, kuwashambulia kwa visu na mawe kisha kuwatupa kwenye dimbwi na kuwamwagia petroli kisha kuwachoma moto.

Katika tukio hilo, kinara wa mauaji walikuwa ni watu wanne lakini shahidi muhimu aliyeshuhudia mauaji hayo, aliwatambua Massawe na mtu mwingine aliyetajwa kuwa ni Bombo Kimario, ambaye hata hivyo polisi hawakufanikiwa kumkamata.

Hukumu hiyo ya kunyongwa hadi kufa, imetolewa leo Jumanne Mei 21, 2024 na Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.

Amesema kuna kanuni ya msingi inayoeleza wazi kuwa mshtakiwa huchukuliwa hana hatia mpaka pale anapotiwa hatiani na chombo chenye mamlaka.

Jaji amesema haki hiyo imo katika ibara ya 13(6) ya Katiba ya Tanzania na bila kuheshimiwa, ndio watu hujichukulia sheria mkononi na kujeruhi na kuua wanaowashuku kutenda makosa kama ilivyotokea katika tukio hilo la mauaji.

“Kwa hiyo kundi hilo linapoka mamlaka ya polisi, mwendesha mashitaka, Jaji na kutekeleza adhabu wanayojichagulia dhidi ya mshukiwa. Hali hiyo ni potofu kwani mshukiwa anakosa haki yake ya kujitetea kwa kosa analotuhumiwa,”amesema Jaji.

Tukio la mauaji lilitokea Februari 9, 2022 huko Kibosho, marehemu hao wawili, Ombeni Mmasi na Marios Mmasi ambao ni ndugu, waliuawa na kundi la watu waliowatuhumu kuwa wezi wa pikipiki.

Ushahidi wa mauaji huu hapa

Shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka, Jackson Munishi ambaye ni shahidi aliyeshuhudia mauaji, anasema siku hiyo alikuwa amekwenda Kibosho Umbwe kuwasalimia watoto wake, na saa 12:00 jioni akaelekea kituoni kupanda basi.

Alipofika eneo la Weremi aliona watu wengi wamekusanyika, alisogelea hadi walipokuwepo ili kuona nini kinatokea, ambapo alimuona na mjomba wake ambaye alimtambua kuwa ni Ombeni Mmasi akishambuliwa na watu.

Kulingana na ushahidi wake, watu waliokuwa wakimshambulia walikuwa ni wanne lakini alifanikiwa kumtambua Valerian Boniface (mshitakiwa aliyehukumiwa kunyongwa) na Bombo Kimaro na hakuweza kuwatambua watu wawili waliobaki.

Ameeleza kuwa aliwaona washitakiwa wakimshambulia ndugu yake huyo kwa kumpiga kwa ngumi na mateke na kisu maeneo ya nyuma ambapo alimuona mjomba wake akidondoka chini na watu hao waliendelea kumshambulia.

Hakuweza kuingilia kati kutokana na ukubwa wa kundi hivyo aliamua kuwapigia simu polisi na akaeleza wakati mjomba wake akiendelea kushushiwa kipigo, alitokea kaka wa Ombeni (Marios) na kuingilia kati kumwokoa mdogo wake.

Shahidi huyo ameieleza Mahakama kuwa alimsikia Marios akiuliza kwa nini wanampiga ndugu yake, ndipo akajibiwa na Bombo Kimaro kuwa kama yuko upande wa mdogo wake, naye wangempiga na hapo walianza kumshambulia.

Amesema aliwaona watu hao wakiwa na fimbo wakiendelea kumshambulia Marios kichwani na aliwaona wote wakiwa wamelala chini hawapumui hapo akajua wamekufa kwa kuwa walikuwa hawajigusi tena wala kuwa na dalili ya uhai.

Kwa mujibu wa ushahidi wake, Massawe na Bombo na washirika wao walishirikiana kuwabeba marehemu na kwenda kuwatupa kwenye shimo na hapo aliwaona wakikusanya majani ya ndizi na kuwafunika nayo kwa juu.

Kisha alimuona Bombo akichukua petroli kutoka kwenye pikipiki na kumwagia juu ya majani yaliyokuwa juu ya ndugu hao kisha akachukua kibiriti na kuwalipua na kukatokea mlipuko mkubwa wa moto uliowaunguza ndugu zake hao.

Shahidi wa pili, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Leonce Mwamunyi ameeleza namna alivyopokea simu kutoka kwa shahidi wa kwanza na kufika hadi eneo la tukio kati ya saa 2:00 na saa 2:30 na kukuta kundi la watu ambao walikimbia.

ASP Mwamunyi amesema watu waliokuwepo eneo la tukio waliwaeleza kuwa kulikuwa na tukio la wizi wa pikipiki uliofanywa na marehemu na kwamba pikipiki hiyo iliyokuwa imeibwa, ilikuwa ikiuzwa na ndugu hao wawili.

Shahidi huyo ameiambia Mahakama kuwa shahidi wa kwanza wa jamhuri aliwatajia polisi kuwa miongoni mwa waliotekeleza mauaji hayo ni Valerian Massawe na Bombo Kimaro kwa kuwa alishuhudia kila kitu.

Shahidi wa nne aliyekuwa mpelelezi wa kesi, Sajini Hassan mwenye namba E.7657 alielezea alivyopewa jukumu hilo ambapo Februari 12,2022 alipata taarifa kuwa Valerian ambaye ni mmoja wa waliotekeleza mauaji yuko baa ya 711.

Akiwa ameongoza na timu ya makachero wa jeshi hilo, walikwenda eneo hilo na kufanikiwa kumtia mbaroni mshitakiwa ambapo baadaye waliendesha gwaride la utambuzi na shahidi wa kwanza, Jackson Munishi aliweza kumtambua.

Alivyojitahidi kujinasua na kitanzi

Katika utetezi wake, Valerian Massawe aliyekuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea, Boniphace Massawe, alisema Februari 9 alikuwa shambani kwake Mailisita na mchana akiwa karibu na nyumbani kwake, alisikia watu wakisema kuna watu wameuawa.

Baadaye alikutana na mmoja wa watu waliompa taarifa aliyemtaja kwa jina la Prosper Massawe ambaye alimkodi ili ampeleke eneo la mauaji na kwa vile yeye pia ni dereva bodaboda, alimpeleka hadi eneo kulipotokea mauaji hayo.

Ameeleza kuwa baada ya siku tatu kupita, miili ya marehemu ilirudishwa kijijini kwa ajili ya mazishi na yeye alishiriki mazishi hayo lakini baadaye alikamatwa na polisi na kuhusishwa na mauaji na anadhani alihusishwa kwa kuwa ni dereva bodaboda.

Amejitetea kuwa anamfahamu shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka (Jackson) kwa vile alizaliwa kijijini hapo na wakakua pamoja na akasema ana sababu mbili anazoamini ndizo zilizomfanya akamtaja kwenye mauaji hayo.

Sababu ya kwanza kwa mujibu wa Valerian ni kuwa kulikuwa na mwanamke aitwaye Light ambaye alimkataa kimapenzi shahidi huyo wa kwanza wa jamhuri na kuhisi kuwa yeye ana mkono katika jambo hilo hivyo kuibua kutokuelewana.

Mbali na sababu hiyo, lakini alisema sababu ya pili ni kuwa mwaka 2021, shahidi huyo alipigiwa kura kijijini kuwa ni mwizi na baada ya kura hiyo, alijenga hisia kuwa ni yeye ndio ameshiriki kula njama na kumfanya apigiwe kura 51.

Katika hukumu yake, alisema upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha shitaka dhidi ya mshitakiwa pasipo kuacha mashaka kuwa hakuna mtu mwingine zaidi yake aliyeshiriki kufanya mauaji kutokana na namna alivyoweza kutambuliwa.

Jaji aliukataa utetezi wa mshitakiwa kuwa hakuwepo eneo la tukio kwa sababu kwanza hakutoa taarifa mapema ya kuegemea Ushahidi huo na pili, ushahidi wake huo ulikosa Ushahidi wa kumuunga mkono hivyo hauaminiki na ni wa mashaka.

Kuhusu utetezi wake kuwa alitajwa tu kwa sababu yeye ni dereva bodaboda, jaji alisema utetezi wake haukuungwa mkono na ushahidi mwingine wowote kuwa ile kuwa bodaboda tu, ndio kulilazimisha yeye kukamatwa na polisi na kushitakiwa.

Pia, kuhusu kura iliyopigwa kijijini, jaji alisema japokuwa hoja hiyo haikuthibitishwa kwa ushahidi kwamba mkutano huo uliwahi kuwapo, mshitakiwa hakueleza ni namna gani shahidi alimjengea chuki pekee kati ya watu 51 waliompigia kura.

Kuhusiana na mwanamke ambaye mshitakiwa alidai shahidi alikuwa anamtaka kimapenzi na alimkataa, mshitakiwa alisema aliripoti mgogoro huo kwa mwenyekiti wa kitongoji ambaye mahakamani alimtaja kwa jina moja tu la Priscus.

Hata hivyo, jaji alisema kwa kuwa mshitakiwa hakumuita mwenyekiti huyo kama shahidi wake ili aieleze Mahakama kama kulikuwepo na kutokuelewana baina ya shahidi na mshitakiwa , anashindwa kuunganisha sababu hiyo na kosa linalomkabili.

Baada ya uchambuzi wa ushahidi kwa jumla wake, jaji alisema ameridhika kuwa upande wa mashitaka umethibitisha shitaka linalomkabili pasipo kuacha shaka hivyo anamtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Related Posts