Dar es Salaam. Kama unakunywa maziwa yaliyotoka moja kwa moja kwa mfungaji yakiwa yamefungashwa kwenye chupa za plastiki haupo salama kiafya.
Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) imetaja magonjwa hatari yanayoweza kumpata mnywaji ni pamoja na tatizo la mimba kutoka ambalo huwapata ng’ombe.
Kwa mujibu wa TDB asilimia tano hadi 30 ya ng’ombe wana vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa mimba kutoka, asilimia 10 hadi 20 tatizo la kifua kikuu na asilimia 10 hadi 20 ya maziwa hayo yana uchafu, hivyo kutokana na tahadhari ya kiafya kutochukuliwa mnywaji anaweza kupata maradhi hayo kupitia maziwa.
Suluhisho pekee la kunywa maziwa salama bodi hiyo imesema ni muhimu kutumia yaliyotoka viwandani kwani ni salama kutokana na taratibu za kiafya kufuatwa kwenye maandalizi.
Usalama wa maziwa ya viwandani japo zipo taarifa kuwa yanaongezwa kemikali, TDB imesema hakuna chochote kinachoongezwa badala yake huchemshwa, kupoozwa na kuhifadhiwa.
Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Profesa George Msalya amesema hayo leo Mei 21, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye semina kwa waandishi wa habari iliyolenga kuwajengea uelewa juu ya umuhimu wa kuielimisha jamii kutumia maziwa kutoka kwa wadau waliosajiliwa na bodi hiyo kulinda usalama wa afya zao.
Kuhusu matumizi ya chupa za plastiki ambazo huokotwa na kusafishwa kuhifadhia maziwa amesema:
“Hatari yake ni kuchangia mtu kupata saratani, vipo vyombo vya kubeba na kuhifadhi maziwa, ni vile vya aluminiamu ambavyo vimeidhinishwa na TDB. Hizi chupa ni kwa ajili ya maji na siyo salama kuhifadhi maziwa,” amesema.
Akizungumzia usalama wa maziwa ya viwandani, Ofisa Maendeleo ya Biashara Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Edmund Mariki amesema maziwa yasipopita kiwandani na mtu akayatumia athari inaweza kujitokeza kama ng’ombe ametumia dawa na ana maradhi.
“Maziwa yanayopita viwandani ni salama zaidi kwa sababu wanabaini ubora kabla ya kupeleka kwa mlaji, yakiwa na shida hayawezi kuhifadhiwa kupelekwa kwa mlaji,” amesema.
Kuhusu uchemshaji wa maziwa, Mariki amesema kitaalamu huchemshwa kwa dakika 30 kwa nyuzi joto 65 kutokana na vimelea vilivyopo kwenye maziwa hupoteza uhai kwa joto hilo.
Amesema uchemshaji wa maziwa hayo hufuata kanuni maalumu ambazo kwa mtu aliye nyumbani anayehitaji kuchemsha maziwa kuua vimelea hupaswa kutenga chombo maalumu chenye maji na kutumbukiza chombo kingine chenye maziwa, kuchemsha kwa joto hilo taratibu na baadaye kuyapooza na kuyahifadhi kwenye jokofu.
Profesa Msalya amesema unywaji maziwa na uzalishaji wake nchini bado hauridhishi, kitendo ambacho kinaifanya Serikali kuagiza maziwa kutoka nje ya nchi.
Amesema kwa mwaka mtu hunywa lita 67.5 za maziwa lakini mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ni mtu mmoja kunywa lita 200 kwa mwaka.
Amesema uzalishaji wa maziwa nao umedorora nchini akieleza mahitaji ya bidhaa ni lita bilioni 12 kwa mwaka na upungufu ni lita bilioni tisa.
Kati ya ng’ombe waliopo nchini milioni 37, amesema ni milioni 1.3 pekee ndiyo hufaa kwa uzalishaji wa maziwa, huku idadi iliyosalia wakikosa sifa ya kufanya hivyo.
“Watu wanapenda kunywa maziwa ya nje zaidi ya ndani. Mwaka 2010 hadi 2020 tuliingiza nchini lita milioni 297 na tulitumia Sh263 bilioni. Mwaka 2023 maziwa yaliyoingizwa nchini kutoka nje yalikuwa lita milioni 11 tukitumia Sh23 bilioni,” amesema.
Ofisa Jinsia na Lishe, Ruth Mkopi amesema maziwa yana madini ya protini ambayo husaidia katika ukuaji na ulinzi wa chembe hai zinazoimarisha afya ya ubongo na moyo.
“Maziwa yana madini chokaa yanayoimarisha afya ya meno na mifupa, madini ya vitamini B2, A, potasiamu ambayo ni muhimu kwa afya ya moyo. Yana kiasi cha kutosha cha madini B12 yanayohitajika na mtu mzima kwa ajili ya utengenezaji wa damu na kuzuia upungufu wa damu, husaidia kuimarisha kinga ya mwili,” amesema.
Meneja Ufundi Maziwa TDB, Deorinidei Mng’ong’o amesema chanzo cha maziwa kuharibika ni kutozingatiwa usafi wa ng’ombe anayekamuliwa.
Uchafu wa mkamuaji, kuongezwa maji kwenye maziwa, vyombo vya kuhifadhi na kusafirisha maziwa.
Bodi imesema wiki ya maziwa nchini itaadhimishwa Mei 28 hadi Juni Mosi na maadhimisho kitaifa yatafanyika mkoani Mwanza.