Majaliwa: Vyombo vya habari kemeeni kauli za ubaguzi

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amevitaka vyombo vya habari vya mitandao ya kijamii kukemea kauli ya aina yoyote ya ubaguzi inayolenga kulipasua Taifa.

Amesema Tanzania imejipambanua kwa kulinda tunu za umoja, amani na mshikamano, hivyo mitandao ya kijamii ina nafasi kubwa ya kuhakikisha inaunga mkono jitihada za kuzilinda.

Majaliwa ameeleza hayo leo Jumanne Mei 21, 2024 alipozindua kongamano la Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii (Jumikita), lililohudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

“Tumeanza kuona mmojammoja wakizungumza ukanda, ukabila, utaifa, Uzanzibari na Utanzania Bara. Hii si sawa, Tanzania ni moja, sote ni Watanzania.”

“Misingi hii imejengwa kwa miaka mingi na viongozi na waasisi Hayati Julius Nyerere na Abeid Aman Karume, ni jambo lililotufanya tuwe pamoja,” amesema Majaliwa.

Ametoa mfano wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Suzan Kunambi kwamba yupo Unguja, lakini asilia yake Mlimba mkoani Morogoro.

Mei 19, 2024 Kamati Kuu ya CCM ilimteua Kunambi kushika wadhifa huo, nafasi iliyoachwa wazi na Jokate Mwegelo aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM).

Kuhusu mitandao ya kijamii, Majaliwa amesema: “Tunatambua na kuthamini mchango wenu na Serikali inaendelea kufungua milango kwenu mje na kushauri namna bora ya kufanya shughuli zenu,” amesema.

Amesema Serikali inatambua jitihada nzuri zinazofanywa na mitandao ya kijamii, hivyo ametumia kongamano hilo kuwataka wamiliki wa vyombo vya habari vya mitandaoni waliopo nje ya jumuiya hiyo kuingia ili kuwa kitu kimoja.

Majaliwa amesema Serikali inafanya jitihada kukuza ajira ikiwemo kuimarisha sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), iliyowawezesha vijana kujiajiri kupitia sekta ya mitandao ya kijamii.

“Miradi mikubwa inayotekelezwa tumeiwekea masharti ya kwamba asilimia 90 wachukue wazawa ili kutengeneza fursa ya Watanzania kujipatia kipato. Pia kwenye maeneo ya viwanda vinachukua wasomi wataalamu wa ngazi mbalimbali,” amesema Majaliwa.

Waziri Nape amesema sekta ya habari imepiga hatua sasa tofauti na miaka iliyopita, akiwataka wanahabari wa mitandao ya kijamii kutumia fursa hiyo kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya maadili.

Nape amewataka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kutenga siku moja  kila mwezi ili kuwajengea uwezo wanahabari wa mitandaoni ili kufuata misingi bora ya kihabari.

Mwenyekiti wa Jumikita, Shaaban Matwebe amesema lengo la kongamano hilo ni kujadili fursa na changamoto katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia kumekuwa na uhuru wa sekta hii, tumepata pumzi wadau, ndiyo maana leo tupo hapa pamoja,” amesema Matwebe.

Ameiomba Serikali kuwapa kipaumbele wanahabari wa mitandao ya kijamii ikiwemo katika huduma za matangazo.

Pia ameomba wapatiwe mafunzo, ombi lililokubaliwa na Waziri Nape na kusisitiziwa na Majaliwa.

Related Posts